HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB) WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA KUJADILI MATUMIZI YA TAKWIMU ZA UMASKINI NA NAMNA BORA YA KUPIMA HALI YA UMASKINI AFRIKA, KATIKA UKUMBI WA KIMATAIFA WA MIKUTANO WA MWL. NYERERE, TAREHE 7 8, FEBRUARI, 2017, DAR ES SALAAM Mhe. Roeland Vande, Balozi wa EU Nchini Tanzania; Mama Bella Bird, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayewakilisha Tanzania, Malawi, Burundi na Somalia; Dkt. Gero Carto, Mwakilishi wa Benki ya Dunia kutoka Roma; Wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa; Viongozi Waandamizi wa Serikali mliopo katika Ukumbi huu; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Mtakwimu Mkuu, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar; Wataalam wote wa Takwimu kutoka Ndani na Nje ya Tanzania; Waandishi wa Habari; Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana. Awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi yetu amani. Amani, utulivu na umoja wetu ndiyo tunu kubwa ambayo inatupatia fursa ya kuwa wenyeji wa mikutano ya kimataifa kama mkutano huu wa leo ambao ni mahsusi kwa ajili ya kujadili matumizi bora ya takwimu zinazohusu mwenendo wa umasikini katika bara letu la Afrika. Ninawapongeza kwa dhati waandaaji wa mkutano huu kwa kuchagua mada muhimu sana kwa ajili ya kujenga ustawi na maendeleo endelevu ya wananchi wetu katika bara la Afrika. Nasema hivi kwa sababu kazi ya kuondoa umasikini ndiyo ajenda mama katika nchi zetu ili kujenga Afrika tunayoitamani, yaani Afrika yenye neema kama ilivyobainshwa katika Ajenda ya 2063 (Agenda 2063: The Africa we want). Umuhimu wa Mkutano huu ndiyo umenifanya nisafiri kutoka Dodoma ambako kikao cha Bunge kinaendelea kuja kushiriki japo sehemu ya uzinduzi wa mkutano. Kwa niaba ya Serikali Tanzania, napenda kuwakaribisheni nyote kwenye Mkutano huu wa Kimataifa wa siku mbili ambao nimeambiwa una washiriki takriban 150 kutoka ndani na nje ya Nchi. KARIBUNI SANA TANZANIA na karibuni katika Jiji la Dar es Salaam (The Harbour of Peace). Nimeelezwa kuwa lengo kuu la Mkutano huu ni kuwakutanisha wataalam mbali mbali kutoka pande zote za dunia chini ya uratibu wa Benki ya Dunia kujadili: (i) matumizi ya taarifa za ufuatiliaji wa hali ya umaskini katika Sera za Nchi ikiwemo Tanzania; na (ii) njia bora zaidi ya kupima hali ya umaskini ili iendane na dhana nzima ya viashiria 1
vilivyoanishwa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo ya mwaka 2030. Wote mnafahamu kuwa kuna Malengo 17 ambayo tuliyaridhia kimataifa mwaka 2015 na katika hayo, lengo la Kwanza ni Kuondoa Kabisa Umaskini wa Mahitaji ya Msingi na Chakula ifikapo mwaka 2030. Nitumie nafasi hii kusema wazi kuwa tafsiri ya umaskini na namna ya kuupima umasikini hasa katika Nchi zinazoendelea imeendelea kuwa changamoto hususan kwa sisi Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia sera za uchumi katika Nchi zaafrika Kusini mwa Jangwa Sahara. Kwa mfano, hivi karibuni kule Bungeni Dodoma, nilitumia takwimu za umasikini kimkoa (basic needs poverty line by region) na lengo langu lilikuwa ni kubainisha mikoa ambayo ni masikini zaidi hapa nchini. Katika mjadala uliofuata baadhi ya wabunge hawakukubaliana kama takwimu hizo kweli zinaakisi hali halisi ya kiwango cha umasikini katika mikoa yao ikilinganishwa na mikoa mingine. Aidha baadhi ya wabunge waliitaka Serikali kuja na programu maalum kupiga vita umasikini katika mikoa hiyo masikini zaidi. Naomba nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Benki ya Dunia na ninyi mabingwa wa takwimu mnaoshiriki katika mkutano huu kuangalia upya moduli mbali mbali zinazotumika katika kupima hali ya umaskini katika Nchi zetu hizi ili kutuwezesha kubuni mikakati ya uhakika ya kupambana na umasikini katika nchi zetu. Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana Sote tunafahamu kuwa lengo kuu la Serikali yoyote duniani ni kuhakikisha kwamba, Wananchi wake wanaishi maisha bora zaidi na yenye neema na kipato cha kumudu gharama za mahitaji ya msingi (chakula, mavazi, makazi, elimu, afya, maji, umeme, usafiri, mawasiliano n.k). Kwa upande wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sisi tumedhamiria kuinua kipato cha Wananchi wetu maskini kwa kuweka nguvu zaidi katika sekta ya Viwanda, hasa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vinatumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini na hasahasa kutokana na kilimo cha mazao, mifugo, uvuvi na madini mbalimbali. Sisi tunaamini kuwa viwanda vinavyoongeza thamani ya kila tunachozalisha ndivyo vitatupatia ajira za kutosha na hususan kwa vijana ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya watu wote Nchini. Ni wazi kuwa utekelezaji wa azma hii ya Serikali itahitaji takwimu bora ili kuweza kufuatilia kama kweli mkakati huu unazaa matunda yaliyokusudiwa kwa maana ya kupunguza kwa kiwango kikubwa hali ya umasikini hapa nchini. Napenda nitumie fursa hii kusisitiza kuwa umaskini wa kipato na chakula ni changamoto kwa dunia nzima na hasa kwa nchi za bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuwa juhudi za ziada zinahitajika ili kukabiliana na changamoto hii. Kwa mujibu wa Takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2013 asilimia 10.7 ya watu wote duniani (7.1 Bilioni) walikuwa wakiishi chini ya dola 1.90 kwa siku ikilinganishwa na asilimia 12.4 mwaka 2012. Hata hivyo, pamoja na takwimu hizi za kuendelea kushuka kwa kasi ndogo ya umaskini duniani, mafanikio haya hayajaonekana wazi kwa baadhi ya Nchi zinazoendelea na hususan kwa Nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania hususan kutokana na ukweli kuwa 2
ukuaji wa uchumi wa nchi zetu unatoka zaidi kwenye sekta zinazoajiri wananchi wachache tena nyingi zikiwa zimejikita mijini sambamba na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu. Takwimu hizo zinaonesha kuwa, umaskini bado ni changamoto kwa watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara ukilinganisha na maeneo mengine ya dunia. Katika kipindi cha mwaka 2013 umaskini katika eneo hili ulipungua kwa asilimia 4 hivyo watu milioni 389 walikuwa bado wanaishi kwa kipato cha chini ya dola 1.90 kwa siku. Hii ina maana kuwa zaidi ya nusu ya watu maskini duniani walikuwa wanaishi Kusini mwa Jangwa la Sahara (chini ya dola 1.90 kwa siku). Taarifa hizi zinaonesha kuwa, wengi wa watu hawa maskini duniani wanaishi maeneo ya vijijini na hawana elimu ya kutosha, na zaidi wamejiajiri katika sekta ya kilimo ambapo zaidi ya nusu ni watoto wenye umri chini ya miaka 18. Ni dhahiri kuwa upimaji wa hali ya umaskini kwa kutumia kigezo cha Dola za Kimarekani 1.90 kwa siku kina changamoto zake baina ya Nchi na Nchi. Dkt. Blandina ameeleza baadhi ya changamoto na mimi naziunga mkono. Kuna baadhi ya vigezo vinavyotumika vingi havieleweki kwa wananchi wetu. Miasamiati mingi inayotumika kama Gini Coefficient wananchi wetu hawaelewi. Hivi kwa nchi kama Tanzania yenye ardhi ya kutosha ambayo kila Mwananchi anamiliki kipande cha ardhi na ambacho anaweza kukitumia kwa lengo la kustawisha kaya na kupunguza umaskini Je, kwanini tusihuishe kigezo cha US$1.90 kwa siku kisihuishwe kuzingatia umiliki wa ardhi? Kadhalika, naamini umiliki wa vifaa kama vile gari, nyumba, na vitu vingine vyenye thamani kubwa katika ngazi ya kaya navyo vinaweza kutumika kuhuisha vigezo vya umaskini. Hili ninawaachia nyinyi watalaam kutafakari kwa kina namna bora zaidi ya kupima umasikini katika mazingira ya nchi zetu. Utafiti wa mwisho wa Mapato na Matumizi ya Kaya uliofanyika Tanzania mwaka 2011/12 na ambao ulitupatia takwimu rasmi za hali ya umaskini hapa Nchini ulionesha kwamba, asilimia 28.2 ya Wananchi wote walikuwa na umaskini wa mahitaji ya msingi na chakula. Kiwango hiki cha umaskini kilipungua kutoka asilimia 38.6 mwaka 1990. Nimeelezwa utafiti mwingine unaandaliwa mwaka 2017/18 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Nitapenda kuona utafiti unajibu maswali yangu niliyoyauliza hapo juu na baadhi ya wenzangu. Nina imani kubwa kuwa tukitumia tafsiri pana zaidi za umasikini kama nilizozitaja hapo juu ni dhahiri tutaona mabadiliko makubwa katika umaskini wa mahitaji ya msingi yakiwemo ya chakula. Ninasema hivi kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano, na kama zilivyokuwa kwa awamu zilizotangulia imejipanga kuendelea na juhudi za kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha Wananchi 3
kukuza uchumi na kupunguza umaskini katika kaya zao. Juhudi kubwa inayofanyika ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa Nchi yenye uchumi wa kati unaotegemea zaidi viwanda ifikapo mwaka 2025. ; Kabla sijahitimisha maelezo yangu nitoe rai yangu kwenu kama ifuatavyo: Kwanza; kama mnavyofahamu uchumi wa Nchi ya Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 7.0 kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu sasa na kupunguza umasikini wa kipato hadi asilimia 28.2. Nina imani kuwa fursa zinazotokana na ukuaji huu wa uchumi huu ndizo zimetufikisha hapa tuliko na niwaombe tuendelee kutumia fursa zinazopatikana katika nchi zetu zinatumika ki-ukweli katika kuleta Maendeleo tunayotaka kuyaona. Pili; Viongozi tuliopewa dhamana ya kusimamia uchumi wa Nchi zetu na kuinua kipato cha Wananchi maskini tuendelee na dhana nzima ya kutumia takwimu bora ambazo ndizo macho na masikio ya Serikali yoyote ile duniani. Sisi Mawaziri wa Fedha na Uchumi katika Kikao cha Nane cha Umoja wa Afrika kilichofanyika Machi mwaka 2015 wote kwa pamoja tuliazimia kutumia takwimu rasmi katika kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya Bara la Afrika na tulienda mbali zaidi kuwa kila bajeti ya Taifa ni lazima tutenge asilimia 0.15 ya bajeti yote kwa ajili ya kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo. Ninawaomba wenzangu kuwa tulitekeleze azimio hili. Tatu; napenda nitumie fursa hii kuwaomba watalaam mlioko hapa kutoka Nchi mbali mbali kuhakikisha kuwa mnatumia vigezo vya ndani ya Nchi (country specific definitions) na vya kimataifa kwa lengo la kutoa taswira nzima ya hali ya umaskini katika Nchi na mwendelee kuelimsha matumizi ya takwimu bora katika kupanga maendeleo ya Wananchi wa Afrika na dunia kwa ujumla. Hili ni jukumu lenu mlioko hapa kuhakikisha mnafuatilia Mipango-mikakati ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya takwimu bora na za wakati. Ninapoelekea kumalizia hotuba hii ya ufunguzi napenda kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuleta Mkutano huu wa Kimataifa Nchini Tanzania na Balozi wa EU hapa Nchini kwa kuendelea kuisadia Tasnia ya Takwimu kupitia Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu Tanzania. Serikali kwa upande wake inaahidi kuendelea kusaidia taasisi zetu za takwimu bara na Zanzibar na taasisi za mafunzo ya takwimu kuziwzesha zifanye kazi yake ipasavyo. Mwisho, napenda kuwaambia wageni wetu kuwa sisi Watanzania ni watu wakarimu. Ni watu wa Taifa lenye amani na mshikamano. Dar es Salaam tulipo hivi sasa ni salama kabisa. Aidha nchi yetu ina vivutio vingi vya utalii tena vya kipekee na maarufu ulimwenguni ikijumuisha mbuga za wanyama kama vile Serengeti, Ngorongoro, Mikumi, Manyara, Selous, Katavi na makazi asili ya sokwe mtu (chimpanzees) ya 4
Gombe magharibi mwa Tanzania. Aidha tuna Mlima Kilimanjaro - dari la Afrika (Africa's roof top), fukwe mwanana bahari ya Hindi (pristine beaches along the Indian Ocean) na visiwa vya Unguja na Pemba vinavyounda Zanzibar maarufu kama spicy islands n.k. Nitumie nafasi hii kuwashawishi mtumie fursa ya hii adhimu ya uwepo wenu hapa Tanzania kabla ya kurudi majumbani kwenu mtembelee vivutio hivi. Ninawahakikishia kuwa mtavifurahia na hamtasahau mtakayoyaona maishani mwenu. Naamini baada ya hapo wote mtageuka kuwa mabalozi wa kutangaza utalii wa Tanzania ambao umeendelea kuchangia vizuri katika kukuza uchumi wa Tanzania na kupunguza umaskini. Baada ya maneno haya naomba niseme kuwa Mkutano wa Kimataifa wa Kujadili Matumizi ya Takwimu za Umaskini na namna Bora ya Kupima Hali ya Umaskini Afrika, sasa umefunguliwa. ASANTENI KWA KUNISIKILIZA 5