wasiofaa. Naomba sana kila raia afanye bidii awezavyo kumkaribia Mwenyezi Mungu vile anavyoona inafaa, lakini asipitishe hukumu juu ya wengine.

Similar documents
Mhashamu Askofu Jude Thaddaeus Ruwa ichi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; Mwadhama Policarp Kardinali Pengo,

Information for assessors (do not distribute this page to participants):

UNIVERSITY OF CAMBRIDGE INTERNATIONAL EXAMINATIONS General Certificate of Education Ordinary Level. SWAHILI 3162/01 Paper 1 May/June 2013

Adhabu ya jino kwa jino na Musitakabali wa imani zetu

Azimio la Umoja wa Mataifa Kuhusu Watetezi wa Haki za Binadamu

Ufunguo wa Kutaalamika Haraka

usudi la Maisha Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na kupishana usiku na mchana, kuna kweli ishara kwa wenye akili, ambaye mkumbuke-

Ushindi ndani ya Kristo W. W. PRESCOTT

Watumishi Wa Kristo. Ellis P. Forsman. Watumishi Wa Kristo (Servants Of Christ) 1

Ellen White, waasisi wa Kiadventista,na Sabato Lunar

PDF created with pdffactory trial version

Kuiponya Picha Tuliyonayo Kuhusu Mungu

Theolojia Ujumla. Mike Taylor Semester Munguishi Bible College

April 14, 2016 COUNTY ASSEMBLY DEBATES 52

WEWE NI NANI? Toleo X Toleo Ukweli wa Injeli Toleo 23

Shabaha ya Mazungumzo haya

"ATATOKEA MARA YA PILI, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu." Waebrania 9:28.

United Pentecostal Church June 2017

JUA HAKI ZAKO, SEHEMU YA 1

Roho Mtakatifu Ni Nini?

Kimesanifiwa na:- E.D.Kissuu ECOMM TANZANIA S.L.P ,Dar es Salaam. Simu:

MELKISEDECK LEON SHINE. katoliki.ackyshine.com

MSAMAHA NA UPATANISHO

Nia Dhidi Ya Kristo Je Unamheshimu?

Haja Ya Dini. Author(s): Publisher(s): Translator(s): Category: Topic Tags: Featured Category: Published on Al-Islam.org (

MUNGU ALIUMBA ULIMWENGU 1 WETU NA VYOTE VILIVYO HAI

Agano Lililofunikwa Kwa Damu

KWA NINI SISI SI MADHEHEBU?

TAMKO LA JUKWAA LA HAKI ZA WATOTO (TCRF) KUHUSU HAKI ZA WATOTO KATIKA KATIBA MPYA

Hati ya kuhitimu kisomo Kenya (K.C.S.E)

UTARATIBU WA KANISA. 2 Jambo la kwanza ninalotaka kusema ni kwamba mchungaji. 3 Sisi tunaamini katika Kanisa la kimitume, tukifundisha

IBADA NA UMOJA WA KANISA Na Mchg. Dkt. Msafiri Mbilu

JE, YAWEZEKANA KUISHI BILA KUTENDA DHAMBI?

ORODHA YA WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI SPIKA MHE. PANDU AMEIR KIFICHO. Rais.

MAADHIMISHO YA MIAKA 15 YA FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO

Kifo Na Mbingu. (Death And Heaven) Ellis P. Forsman. Kifo Na Mbingu (Death And Heaven) 1

NGUVU. Utangulizi. Yesu alisema,

walozaliwa, si kwa damu, wala mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, mbali kwa Mungu. Sisi sio tena binadamu wa kawaida tu kwa sababu sisi ni w

Kifo Na Mbingu (Death And Heaven)

Uongozi Siri Na Larry Chkoreff. Version 1.2 Desemba 2010

Inavyodaiwa na wanaochanganya Biblia. Ellis Forsman. Inavyodaiwa na Wanao changanya Biblia (Alleged Bible Contradictions) 1

Ndugu na dada zangu wapendwa,

MACHAGUO YA UZAZI KUFIKIRIA KUWA MZAZI

Maisha Yaliyojaa Maombi

Tora UTANGULIZI KWA TORA SOMO LA KWANZA

KAMA MUNGU YU PAMOJA NASI, BASI YAKO WAPI MATENDO YAKE YA AJABU?

Maisha Ya Mkristo Ni Nini?

MUNGU ANADHIHIRISHWA KUPITIA KWA YESU KRISTO.

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA,KWA WANANCHI, 30 SEPTEMBA, 2001

Elimu ya Msingi inaelekea Upande Sahihi? Kufikiri na Nyerere Rakesh Rajani

Kiu Cha umtafuta Mungu

TANZANIA OSAKA ALUMNI. Kitabu cha Mbinu Bora

GOVERNMENT NOTICE No... PUBLISHED ON THE ELECTRICITY ACT, (CAP.131) ORDER. (Made under Section 23)

Makasisi. Waingia Uislamu

Kutetea Haki za Binadamu

Na Itafunika Wingi Wa Dhambi

RISALA FUPI YA KUMUWEZESHA MTU KUPAMBANUA NI IPI DINI YA HAKI MWANDISHI: SALEH M. KYAMBO

YEHOVA-YIRE 1. 2 Baba yetu wa Mbinguni, tunakikaribia Kiti Chako cha. 3 Tunakushukuru kwa kutuzuru jana jioni. Tunaomba

Human Rights Are Universal And Yet...

LALA. Terry Warford. LALA (Sleep - Terry Warford) 1

GRACE COMMUNION INTERNATIONAL KANUNI YA IMANI

Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini E. S. MOHOCHI University of Egerton, Kenya

Mukhtasari Wa Mabishano Kwa Na Dhidi Ya Vikombe Vingi Vya Ushirika

KANISA NA UAMSHO Na Mchg. Dkt. Faith Lugazia

WAFUNAJI WA NAFSI ABC By Vagn Rasmussen Translation by Lydia Madsen

Kitabu Cha Mafunzo Ya Uongozi Kwa Wanawake

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame M. Mbarawa (Mb.); Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge wote mliohudhuria;

HOTUBA YA WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU: KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU MHE

MIAKA 500 YA MATENGENEZO YA KANISA NA USHUHUDA WETU Na Askofu Dr. Abednego Keshomshahara

Miradi na jamii. 3.1 Utangulizi

B. Wanafunzi watapata ufahamu mkubwa wa kitabu hiki, na jinsi kinavyofundisha kuhusu kanisa.

Azimio lililopitishwa na Mkutano Mkuu tarehe 18 Desemba 2013 [juu ya taarifa ya Kamati ya Tatu (A/68/456/Add.2)]

Ndugu na dada zangu wapendwa,

WAKOLOSAI MTAALA. B. Maoni: Tunapendekeza uwe na fafanuzi (commentary) yoyote yenye kushikilia mafundisho ya awali (conservative) katika Wakolosai.

Mwongozo wa Utamaduni Toleo la Kwanza

MASWALI NA MAJIBU JUU YA KITABU CHA MWANZO

2

Ndugu na dada zangu wapendwa,

Kwa Nini Yesu Alikufa Msalabani?

Tumaini Kwa Afrika. Thomas Schirrmacher. Hoja 66. Dibaji na Prof. Mchungaji Dk. Thomas K. Johnson. Thomas Schirrmacher Tumaini Kwa Afrika TASCM RVB

UNABII WA BIBLIA. CBM Publishing 32 Blenheim Road, Far Cotton Northampton, England. NN4 8NW

Mzabibu Na Matawi. (The Vine And The Branches) Ellis P. Forsman. Mzabibu Na Matawi (The Vine And The Branches) 1

Mwongozo wa Kanisa la Waadventista wa Sabato

JHSPH MAADILI YA KUFANYA UTAFITI WA MASUALA YA BINAADAMU MUONGOZO WA MAFUNZO YA UTAFITI

maombi, kabla tu hatujalifungua Neno hili la Kiungu.

Mafundisho Ya Msingi Wa Kikristo. Na Andrew Connally

Oktoba-Desemba

VITAMBULISHO VITA NO DHA HIRI VYA KA NISA LA KWELI LA MUNGU ALIYE HAI

CONSTITUTION OF KENYA REVIEW COMMISSION (CKRC)

2

ONYO LA MWISHO KWA DUNIA

UZAO WA NYOKA. 2 Basi, usiku huu, tuna malimbuko tu ya utukufu huo mkuu. 3 Kwa uchaji tunasimama kwa imani yetu katika Uwepo

MAHUBIRI TUNAYOWEZA KUONA

Uponyaji Wa Laana. (Kumb. 28:1-14).

CONSTITUTION OF KENYA REVIEW COMMISSION (CKRC)

Silaha Za Shetani. Ellis Forsman. Silaha Za Shetani (The Devices of Satan) 1

IMANI NA MATENDO ELLEN G. WHITE

HISTORIA, MAENDELEO NA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA TANGU UHURU HADI MIAKA HAMSINI YA UHURU 9 DESEMBA 2011.

CONSTITUTION OF KENYA REVIEW COMMISSION (CKRC)

Transcription:

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWENYE IBADA YA KUWEKWA WAKFU NA KUINGIZWA KAZINI ASKOFU MARTIN FATAELI SHAO WA DAYOSISI YA KASKAZINI YA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA, KANISA KUU, MOSHI, 09 MEI 2004 Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Baba Askofu Dkt. Samson Mushemba; Askofu Mpya wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, Baba Askofu Martin Fataeli Shao; Maaskofu Wengine Wote; Wachungaji, Viongozi wa Kanisa na Waumini; Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana: Bwana Asifiwe! Naungana nanyi kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuweka sote hai hadi siku hii ya leo aliyoipanga yeye mwenyewe ya kubadilishana uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwa heshima na taadhima. Ibada imekwenda vizuri sana. Nawapongeza walioiandaa na kuiendesha. Nawashukuru waumini wote walioniombea nilipolazwa hospitalini Uswisi mpaka ikampendeza Mwenyezi Mungu kunusuru maisha yangu. Na kwa yote haya sifa, heshima na utukufu ni kwa Bwana Mungu wetu, kwani: Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwazo mwangaza utokao juu umetufikia, Kuwaangazia wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani. (Luk. 1:78-79) Ndugu Wana-Dayosisi ya Kaskazini: Katika siku hii muhimu, nakuja kwenu na salamu za shukrani na upendo. Ninawashukuruni sana kwa kunialika kwenye ibada hii, na ninashukuru sana kwa mapokezi mema, ya upendo, mliyonipa mimi na Mama Mkapa, na ujumbe wangu wote. Kwa niaba yao wote, nasema ahsanteni sana.

Kwa niaba yao pia nakupongezeni sana Wana-Dayosisi hii kwa kupata kiongozi mpya, aliyepatikana kwa ridhaa yenu, mliyeridhika naye, kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Dayosisi. Kule nje kwenye uwanja wa siasa, baada tu ya uchaguzi, utasikia kesi chungu nzima zinafunguliwa kupinga matokeo, na pengine hata kupakana matope tu. Kwenu mambo ni shwari kabisa. Aliyechaguliwa amechaguliwa, na wengine wote wanakiri hivyo na kuonyesha utii wao kwa kiongozi wao mpya. Laiti mngekuja kutupiga msasa kwenye siasa, ili huko nje nako kuwe na chaguzi za kiungwana kama hizi!! Naungana pia na waliozungumza kabla yangu kukupongeza sana Baba Askofu Martin Fataeli Shao kwa kustahiki heshima hii kubwa, na kuonekana mwenye uwezo wa kiroho na kimwili kubeba mzigo wa kuchunga kondoo wa Bwana. Kwa niaba ya Mama Mkapa, na familia yangu yote; na kwa niaba ya Serikali, nakupongeza sana na kuungana na wote wanaokuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe busara, uvumilivu, na afya ya kubeba mzigo mzito huu. Baba Askofu, Natumia maneno mzigo mzito kwa makusudi. Biblia inawaita viongozi wa kanisa wa ngazi yako kuwa ni wachungaji wa kondoo. Na wewe ndivyo utakavyokuwa. Ukirudi nyuma kwenye historia, wachungaji kondoo walikuwa na maisha magumu. Wale tunaowasoma kwenye Kitabu cha Mwanzo waliishi maisha ya shida, kwenye joto sana misimu fulani na baridi sana misimu mingine. Walipambana na ukame na uhaba wa malisho, na walipigana na wanyama wakali waliokuwa wanavizia kondoo. Hayo ndiyo maisha unayoyaanza leo, Baba Askofu Shao. Yakobo alikuwa mchungaji mwema, japo kazi hiyo aliifanya kama mahari ya kuolea katika nyumba ya Labani. Ninyi viongozi wa dini mnayajua mazingira yaliyomfanya Labani amfanyie fujo Yakobo wakati wakiachana mwisho wa mkataba wake. Lakini, napenda ninukuu maneno ya Yakobo kwa Labani. Alisema ifuatavyo, akielezea rekodi yake ya uchungaji katika nyumba ya Labani: Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala. Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku. Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu. Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara

kumi. Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu ameziona, akakukemea usiku huu. (Mwanzo 31:38 42) Ndugu Wana-Dayosisi, Hayo ndiyo maisha ya mchungaji bora wa kondoo. Maaskofu wanaitwa wachungaji wa kondoo wa Bwana. Wanabeba mengi. Wanavumilia mengi. La muhimu kwao si uhodari tu wa uongozi, bali pia moyo wa upole, uvumilivu, na kuwa tayari kufanya kazi katika mazingira magumu, na kuwalinda kiroho na kimwili wale waliokabidhiwa kwao kuwaongoza. Maneno ya Yakobo akiagana na Labani ni maneno yanayofaa kusemwa na kiongozi yoyote wa Kanisa aliyefanya na kumaliza vizuri kazi yake. Ndugu Viongozi wa Kanisa: Taifa letu halina dini rasmi. Na hivyo Serikali haiko madarakani kupendelea dini au madhehebu yoyote ya dini. Lakini Serikali inatambua na kuheshimu uhuru wa imani ya dini wa kila raia; na inachukulia kwa uzito mkubwa wajibu wake kuhakikisha kila raia anayo haki na uhuru wa kuamini na kuabudu apendavyo ili mradi havunji sheria, na haingilii uhuru wa raia mwingine naye kuamini na kuabudu apendavyo. Nasema hivyo kwa sababu inaonekana wapo watu ambao wanataka Katiba ya Nchi yetu ilinde haki yao peke yao ya kuabudu. Unajua, mambo ya imani ni magumu sana, na nyeti sana. Maana, kila muumini anaamini kwa dhati kabisa kuwa aaminivyo na aabuduvyo yeye ndivyo sahihi, na ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyo na alivyoagiza. Katika hali hiyo, njia pekee ya kuhakikisha amani na usalama katika jamii ni kutoa ruhusa kwa kila mtu kuamini na kuabudu apendavyo, lakini bila kudhihaki, kudharau, kutukana, kubeza au kupuuza imani na ibada za wengine. Naomba sana kila Mtanzania azingatie kanuni na wajibu huo wa kuheshimu imani na ibada za wenzake. Tusiwe wabinafsi. Tusigombane. Tusidharauliane. Maana hakuna binadamu yeyote mwenye ufunguo wa mbinguni. Kwa hiyo hayuko mwanadamu ambaye ataamua nani mwenye haki ya kuingia mbinguni na nani mkosaji wa kwenda kuzimu. Sasa kwa nini tusivumiliane, na tukamwachia Mwenyezi Mungu mwenyewe aamue nani kati yetu mwenye haki na nani mkosaji? Lipo tatizo la msingi katika mambo ya imani za dini. Kwa kadri mtu anavyojihisi amemkaribia Mwenyezi Mungu, au ameokoka, ndivyo anavyokuwa hatarini kutumbukia kwenye mtego wa kushawishika kuwaona wengine kuwa ni wakosefu, waliopotea,

wasiofaa. Naomba sana kila raia afanye bidii awezavyo kumkaribia Mwenyezi Mungu vile anavyoona inafaa, lakini asipitishe hukumu juu ya wengine. Kazi hiyo tumwachie Mwenyezi Mungu. Ndugu Viongozi wa Kanisa, Kama ilivyo kawaida yangu, nipatapo fursa kama hizi, napenda kutambua, kwa shukrani, mchango wa mashirika ya dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi yetu. Leo pia napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa mchango wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania kwenye ujenzi na uendeshaji wa huduma za jamii. Na kwa njia ya pekee nampongeza na kumshukuru Baba Askofu, Dkt. Erasto Kweka, ambaye katika miaka yake yote ya uongozi wa Dayosisi hii amekuwa mkereketwa mkubwa, kwa imani na kwa vitendo, wa maendeleo kwa jumla, lakini hasa maendeleo ya elimu, afya na maji. Kwa niaba ya Serikali, nakushukuru sana Baba Askofu Dkt. Erasto Kweka, kwa mchango wako mkubwa, na ushirikiano wako. Kwa pamoja tumefanya kazi kubwa kwa maendeleo na ustawi wa wananchi katika Dayosisi yako na kwingine. Unayo haki kuyaonea fahari mafanikio hayo. Napenda kumhakikishia Askofu mpya, Baba Askofu Martin Fataeli Shao, kiwango hicho hicho cha ushirikiano tulichokupa wewe, ili kwa pamoja tudumishe na kuendeleza kazi nzuri ya Kanisa kwa maendeleo na ustawi wa wananchi. Baba Askofu: Tunashirikiana vizuri kwenye mambo mengi. Lakini napenda kujenga hoja ya kushirikiana pia katika kubadilishana mawazo. Ni jambo la kusikitisha kuwa yapo matatizo mengi duniani ambayo chanzo chake ni kukosekana kwa mawasiliano na majadiliano baina ya watu au taasisi mbalimbali. Binadamu tumeumbwa tofauti, tukakulia katika mazingira tofauti, tukaelimika tofauti, na tukapewa majukumu tofauti hapa duniani. Haiwezekani tukawa na uelewa au uzoefu sawa wa kila jambo, au tukawa na mtazamo mmoja. Mimi ninaamini kuwa, ukiacha kando yale mambo ya kiroho, kwenye mengine yote yaliyobaki hakuna sababu ya kutokuwa na mawasiliano, mashauriano, na kubadilishana mawazo baina ya Serikali na viongozi wa dini katika ngazi mbalimbali. Hapo ndipo kila upande utauelewa vizuri upande mwingine, na hasa kuelewa chanzo cha tofauti za mtazamo na mikakati. Maelewano ni mwanzo mzuri wa ushirikiano na kuheshimiana, hata pale ambapo hatukubaliani kwa kila jambo. Inawezekana, na wala si ajabu, yakatokea mambo ya kiserikali yasiyowapendeza viongozi wa dini. Pengine kwa sababu za kweli, za msingi; lakini pia pengine kwa kutoelewa undani wa jambo lenyewe na mazingira

yake. Inawezekana pia wakati mwingine yakawepo mambo ya kidini yasiyowapendeza viongozi wa Serikali. Pengine kwa sababu za kweli, za msingi; lakini pia pengine kwa kutoelewa undani wa jambo lenyewe na mazingira yake. Katika hali hiyo, ushauri wangu ni kuwa uwepo utaratibu na tabia kwa viongozi wa dini na wale wa Serikali kujadiliana zaidi, badala ya kusemana zaidi. Mimi nina uhakika kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye serikali zipo madarakani kwa ridhaa yake, atapendezwa zaidi akiona viongozi wa dini na viongozi wa Serikali wakiwa wabia wa kweli katika kuwahudumia viumbe wake. Hakuna raia wa kawaida, wa dini yoyote au dhehebu lolote la dini, ambaye atafaidika kwa magomvi kati ya Serikali na viongozi wa dini. Ndugu Viongozi wa Kanisa: Tanzania tumepiga hatua kubwa, kuliko Waafrika wenzetu wengine, katika kujenga hisia za utaifa na kuziweka mbele, badala ya kutanguliza hisia za udini, ukabila na umajimbo. Lakini hata kwetu Watanzania, bado unasikia minong ono ya udini, ukabila na umajimbo. Minong ono hiyo inasikika kwenye siasa, hasa tunapoelekea kwenye uchaguzi; na nimesikia, kwa mshangao, kuwa hata kwenye dini ipo minong ono ya ukabila na umajimbo. Nashukuru sana kuwa, kwa ujumla, viongozi wa dini wameungana na Serikali kuonya na kukemea mwelekeo wa kutaka kurejesha mambo ya udini, ukabila na umajimbo katika nchi yetu. Viongozi wa dini wanaheshimika sana kwenye jamii. Kwa hakika Serikali inawaheshimu sana. Viongozi wa dini kwa ujumla ni wasomi na waelewa wa mambo. Kwa heshima wanayopewa, na uelewa tunaoamini wanao, viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa katika jamii. Naomba sana waelekeze ushawishi wao kwa yaliyo mema kwa taifa letu; na usiwe ushawishi wa maneno tu, bali pia ushawishi kwa mfano wa vitendo vyao wao wenyewe. Mtakubaliana nami kuwa yaliyo mema kwa taifa letu ni maendeleo, ni umoja, ni utaifa, ni upendo na ni mshikamano. Na kama hayo ndiyo malengo yetu sisi sote, kwenye dini na kwenye siasa, lazima tutumie majukwaa yote, ya dini na siasa, kuhubiri na kushawishi uimarishaji wa taifa letu kwa kukataa mambo yanayodhoofisha umoja wetu, kama vile udini, ukabila na umajimbo, na kuhimiza yale tu yaliyo mema kama vile maendeleo, umoja, utaifa, upendo na mshikamano. Ushawishi wetu kwenye siasa kama kwenye dini uwe wa sisi wenyewe kwanza kuamini, kisha kunena na hatimaye kutenda. Kauli zetu na vitendo vyetu viwe na mwelekeo mmoja, na mfano kwa wengine. Nikiwa Mkristo mwenzenu, sisahau maneno ya hekima yaliyo katika Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote:

Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je, ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akamwambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. (Yak. 2:14 17) Ndugu Wananchi: Hali ni hiyo hiyo kwenye mambo ya kidunia. Kwenye majukwaa ya kisiasa, na yale ya kidini, tunaweza kuhubiri sana umoja wa kitaifa; tunaweza kulaani udini, ukabila na umajimbo. Ni muhimu kufanya hivyo, lakini peke yake haitoshi. Lazima kauli hizo zithibitishwe kwa vitendo. Tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani. Na uchaguzi unaweza kuimarisha umoja na utaifa wetu. Lakini ukitekwa nyara na wanaohubiri jambo moja, na kutenda jambo jingine, uchaguzi huo unaweza kuathiri sana umoja na utaifa wetu. Nawasihi sana wanasiasa, na viongozi wa dini: Twende kwenye kipindi cha uchaguzi tukitetea imani yetu ya umoja na utaifa, kwa kauli, lakini hasa hasa kwa vitendo. Kisitokee chama cha siasa, na asitokee mgombea kwenye uchaguzi, kukita kampeni zao kwenye kabila fulani, dini fulani au kanda fulani. Vilevile zisitokee kama ilivyokuwa kwenye baadhi ya chaguzi zilizopita Jumuiya za dini kutumia heshima yao kubwa, na ushawishi wao mkubwa, kuwachagulia wafuasi wao wagombea wanaostahili kuungwa mkono, au chama cha kukipigia kura. Katiba ya Nchi ndiyo imani yetu kitaifa. Kila mtu akiulizwa atasema anaamini binadamu wote ni sawa, kwamba wanastahili heshima, kwamba wana uhuru kwenye mambo ya imani za dini, na mvuto wa kisiasa. Lakini imani hiyo imekufa nafsini mwake kama haijidhihirishi kwa vitendo. Naomba sana twende kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani tukiwa tumeamua kutekeleza imani zetu za usawa, umoja, utaifa, mshikamano na uhuru wa kuamua, kwa vitendo. Ndugu Viongozi wa Kanisa: Namalizia kwa kukupongeza tena Baba Askofu, Dkt. Erasto Kweka, kwa kuhitimisha uongozi wako wa Dayosisi hii na kwa ushirikiano wako. Nakushukuru kwa kunialika mimi na Mama Mkapa kushuhudia unapohitimisha kazi yako kubwa, ya kuongoza Dayosisi hii kwa miaka mingi, na kuikabidhi salama kwa awamu nyingine ya uongozi, ikiwa imepiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiroho na kimwili tangu ulipokabidhiwa kuiongoza. Nakupongeza sana,

na ninakushukuru sana. Pongezi hizi tunazitoa pia kwa Mama Askofu Kweka ambaye nina uhakika amekuwa nguzo yako katika miaka yote hii ya uongozi wako wa Dayosisi hii. Kwa pamoja tunawatakieni mapumziko mema, furaha, afya njema, maisha marefu na baraka tele za Bwana. Nakupongeza sana Baba Askofu Martin Shao kwa heshima hii, na madaraka haya makubwa, uliyopewa. Nampongeza pia Mama Askofu Shao ambaye nina uhakika atakuwa nguzo yako katika uongozi wako. Kwa upande wa Serikali tunakuhakikishia ushirikiano mkubwa sana katika kazi zako. Baba Askofu: Nimeuelezea wadhifa uliopewa leo kuwa mzigo mzito. Nami pia, kwa muda wa miaka 8 na nusu sasa, katika medani nyingine, nimebeba mzigo mzito kama huo. Katika kutekeleza jukumu la mzigo huo, mara kwa mara nimefarijiwa na maneno ya Utenzi wa Roho yafuatayo: HYMN We fish in vain who fish alone And think ourselves the harvest s lord, For we but catch what you have sown In seas we neither make nor own, And have no claim to work s reward. The sea and all their fish are yours, And we your servants at the oar; Then let us work while night endures Until the rising sun assures That you await us on the shore. Twasumbuka bure tuvuao peke yetu Kujidhania sisi ndio bwana wa mavuno, Maana hatuvuni ila ulichopanda wewe Katika bahari tusizoziumba wala kuzimiliki, Na wala hatustahili malipo kwa kazi hizo. Bahari na samaki vyote ni vyako,

Tulichoshika watumishi wako ni makasia; Tufanye kazi basi usiku ungalipo Hadi pambazuko litufariji Kuwa wewe watungoja pwani. Baba Askofu Shao: Namwomba Mwenyezi Mungu azidi kukubariki na kukuongoza, wewe na Mama Askofu Shao, na kukupeni hekima na busara. Ahsanteni kwa kunisikiliza. Bwana Asifiwe!