Lishe na Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI VIDOKEZO MUHIMU KATIKA UNUNUZI NA USALAMA WA CHAKULA

Similar documents
Lishe na Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI

Utangulizi wa ugonjwa wa shinikizo la damu

Information for assessors (do not distribute this page to participants):

PYRINEX. 1 Liter INSECTICIDE

Uwepo, Athari na Udhibiti wa Sumu-Suvu Kwenye Vyakula vya

KILIMO CHA VITUNGUU MAJI NA VITUNGUU TWAUMU (SWAUMU)

Picha ni hati miliki ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Watoto(PCD), Imperial College London. Maelezo

GOVERNMENT NOTICE No... PUBLISHED ON THE ELECTRICITY ACT, (CAP.131) ORDER. (Made under Section 23)

Mfumo na maelezo ya kina ya mpango wa kimataifa wa viwango vya chakula kwa wenye matatizo ya kumeza (IDDSI) Juni 2017

Jamii. ,,,^mm^mmm-<^^^^ illli MA RH-EREN.CE CENTRE

MTI KWA MATUMIZI YA KILA AINA HDRA

Siku ya kwanza. Mguso wa ngozi-kwa-ngozi (Ulezi wa kangaruu) Mtoto wako anaweza kuhisi mdundo wa moyo wako

Njia Bora za Ukusanyaji na Upimaji Maziwa

Njia bora za ukusanyaji na upimaji maziwa

TIST (TANGA) HABARI MOTO MOTO. Kutunza miche yako. Take care of your seedlings. Take care of your trees

pages/mkulima-mbunifu/

Uzalishaji wa mboga na matunda ni muhimu kwa afya na kipato

Utunzaji, Uhifadhi na Usafirishaji Bora wa Maziwa

Jifunze kusimamia pesa zako nchini Uskoti

GOVERNMENT NOTICE No... PUBLISHED ON THE ELECTRICITY ACT, (CAP.131) ORDER. (Made under Section 23)

2 Usimamizi wa Rutuba ya Udongo Tanzania Organic Agriculture Movement

UMRI WA MAKAMO NA KUKOMA KWA HEDHI

Kifaa Maalum cha Kutazamia Jua: Maelekezo ya kutumia

Usindikaji bora wa maziwa

MATUMIZI YA FACEBOOK KWA BIASHARA. Kwa Wanaoanza

KUZALISHA MBEGU YA MAHARAGE KIJITABU CHA KWANZA

Hati ya kuhitimu kisomo Kenya (K.C.S.E)

Bustani 10,000 Katika Afrika. Alberto Prina

Kuwa na Ukimwi ni kama vile kutakiwa kuendelea kuuzima moto unaoniunguza bila kukoma.

TIST HABARI MOTO MOTO

JHSPH MAADILI YA KUFANYA UTAFITI WA MASUALA YA BINAADAMU MUONGOZO WA MAFUNZO YA UTAFITI

Teknolojia za Utayarishaji, Usindikaji na Matumizi ya Matunda na Mboga baada ya kuvuna

International Labour Office. Kazi za Ndani Zenye Madhara kwa Watoto: Kijitabu cha Maelezo Mafupi

Mwongozo wa Kitaifa wa Ujumbe wa Uzazi wa Mpango

Ni kwa nini mkulima awe maskini?

4 WADUDU,MAGONJWA NA MAGUGU

Hatari, Haki za Usalama katika Bahari 03

Mukhtasari Wa Mabishano Kwa Na Dhidi Ya Vikombe Vingi Vya Ushirika

Uhakika wa Mbegu kwa Uhakika wa Chakula MWONGOZO WA UZALISHAJI WA MBEGU ZA ASILI ZA MAHINDI

Wewe Maisha Yako Ndoto Zako. Kitabu cha Vijana Balehe

Kijitabu cha Maelezo cha Programu ya Famasia

HOTUBA YA WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU: KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU MHE

Uzio wa pilipili unazuia tembo kuvamia mazao shambani! Jinsi ya kujenga na kudumisha uzio wa pilipili Tanzania

AMMA KWA AFRIKA RATIBA/ITIKADI. Ratiba Maalum ya Kutibu Magonjwa Maambukizi na Hususan Fikra Zinazoleta Pooza Mwili na Akili

Shamba Darasa na Stadi za Maisha kwa Vijana (SDSMV) Tanzania. Kiongozi Cha Mwezeshaji. Jaap Van Pol na Francesca Dalla Valle

Muongozo wa utatuzi. Kwa wasimamizi wa malaria RDTs 06/11/16. MALARIA Rapid Diagnostic Test

MTIHANI WA MWIGO WA WILAYA YA NANDI KASKAZINI 2013

Upande 1.0 Bajeti yako

Yaliyomo. Kuhusu kitabu hiki. Hautakuwa peke yako. Mfumo wa msaada ni wa manufaa sana wazazi wote wanahitaji!

Misamaha ya kodi Tanzania: Je, ni mikubwa sana na kutufanya tuwe tegemezi kwa misaada?

Mwongozo huu wa ufugaji kuku wa Asilia umezinduliwa rasmi leo tarehe 1 Agosti 2009 wakati wa sikukuu ya Wakulima Tanzania mjini Mbeya

Uzazi wa Mpango. Uzazi wa Mpango. Kulinganisha Ufanisi wa Njia za Uzazi wa Mpango. iwe na ufanisi zaidi. Zenye ufanisi.

TANZANIA MARKETS PAN Sera zinazoboresha masoko

Mutugi Kamundi. Jemma Kahn. Kiswahili. Demane na pacha wake. Author - South African Folktale

MACHAGUO YA UZAZI KUFIKIRIA KUWA MZAZI

Human Rights Are Universal And Yet...

Ufunguo wa Kutaalamika Haraka

Usimulizi wa Riwaya ya Nyongo Mkalia Ini E. S. MOHOCHI University of Egerton, Kenya

SERA & TARATIBU YA YALE NEW HAVEN HEALTH

ONDOA MADINI YA RISASI KATIKA RANGI: LINDA AFYA YA WATOTO

Kuwawezesha wasichana kwa kuboresha kujikubali na kujithamini Hivi Ndivyo Nilivyo

MUONGOZO WA UTUNZAJI WA URITHI WA UTAMADUNI 1 SECURITY AT MUSEUMS

Muhtasari wa taarifa ya warsha ya wataalamu juu ya mfumo wa habari kwa njia ya ramani (PGIS), Morogoro, Juni 30 - Julai 1, 2014

Mwongozo wa Utamaduni Toleo la Kwanza

Wadudu na magonjwa ya mazao

CGAP Smallholder Household Survey in Tanzania / Utafiti wa kaya ndogondogo Tanzania

Vijana wanazungumza kuhusu ujinsia, maisha na uhusiano VIJANA WANAZUNGUMZA KUHUSU NGONO, MAISHA NA UHUSIANO. Training and Research Support Centre

UNIVERSITY OF CAMBRIDGE INTERNATIONAL EXAMINATIONS General Certificate of Education Ordinary Level. SWAHILI 3162/01 Paper 1 May/June 2013

Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu WEMA

Mwongozo wa Jamii juu ya Afya ya Mazingira

KUWEZESHA MBINU ZA UZUIAJI MIMBA KATIKA SUHULA ZA AFYA: MASWALI 10 KWA VIKUNDI VYA JAMII KUZINGATIA

TIST HABARI MOTO MOTO. Benefits of Loan Repayment. Faida za ulipaji wa mikopo U OTESHAJI W A M ITI Y A M ATUNDA

UNACHOHITAJI KUJUA KUHUSU VIKWAZO VYA KULINDA MAISHA KATIKA USAIDIZI WA KIMATAIFA WA AFYA KWA MSAADA WA KIMATAIFA UNAOFADHILIWA NA MAREKANI

MBINU ZA IPM KWENYE KILIMO CHA KAHAWA

KUUNGANISHA VIZAZI KUPITIA RADIO MWONGOZO KUTOKA AFRIKA KWA WAANDAJI WA VIPINDI VYA RADIO WANAOFANYAKAZI NA WATOTO NA VIJANA

Azimio la Umoja wa Mataifa Kuhusu Watetezi wa Haki za Binadamu

Palliative Care Toolkit

Utumiaji Wa Kiswahili Na Lugha Za Jamii Kijinsia Nchini Tanzania Y.P. MSANJILA University of Dar-es-Salaam, Tanzania

UTANGULIZI ANUANI NA MANDHARI YA CHUO

Miradi na jamii. 3.1 Utangulizi

Kilimo cha kiekolojia cha Wakulima Wadogo Hufanikisha Haki za Mazingira

Maoni ya Wananchi juu ya Huduma za VVU na UKIMWI Nchini Tanzania

Ufundishaji wa lugha nyingine

Huduma kwa wateja kupitia barua pepe na ujumbe mfupi Fig

Adhabu ya jino kwa jino na Musitakabali wa imani zetu

Mazoezi yaliyofanyika wakati wa warsha kuhusu Elimu-Jumuishi kwa Vitendo. Zanzibar, 7-10 Februari 2006

Vyote Unavyopaswa Kujua Kuhusu Viazi Vitamu

Makala ya Mshiriki wa Mafunzo

USIMAMIZI MKUU WA UBORA WA MAHURUJI

Sera ya Faragha. Upeo. Aina za Data na Mbinu za Ukusanyaji

MWONGOZO WA UTUNGAJI WA SHERIA NDOGO NA USHIRIKI WA WANANCHI

HALMASHAURI YA WILAYA YA SUMBAWANGA

TAMKO LA JUKWAA LA HAKI ZA WATOTO (TCRF) KUHUSU HAKI ZA WATOTO KATIKA KATIBA MPYA

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA,KWA WANANCHI, 30 SEPTEMBA, 2001

Haja Ya Dini. Author(s): Publisher(s): Translator(s): Category: Topic Tags: Featured Category: Published on Al-Islam.org (

TAFSIRI RAHISI YA MPANGO WA MAENDELEO YA AFYA YA MSINGI (MMAM)

Azimio lililopitishwa na Mkutano Mkuu tarehe 18 Desemba 2013 [juu ya taarifa ya Kamati ya Tatu (A/68/456/Add.2)]

Waandishi: wa Toleo la 5. Scholastica Jullu Athanasia A. Soka Safina Hassan Mary Njau. Toleo la 5: 2008 ISBN

JUA HAKI ZAKO, SEHEMU YA 1

UFUPISHO WA 35. Hali ya kiulimwengu ya Tekinolojia ya kibiashara/ugeuzi jeni na uboreshaji mazao: Clive James Chair, ISAAA Board of Directors

Transcription:

Lishe na Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI VIDOKEZO MUHIMU KATIKA UNUNUZI NA USALAMA WA CHAKULA COUNSENUTH NA HALMASHAURI YA MANISPAA YA ILALA, June, 2004

VIDOKEZO MUHIMU KATIKA UNUNUZI NA USALAMA WA CHAKULA ISBN 9987-8936-8-6 COUNSENUTH, 2004 Kimetayarishwa na: The Centre for Counselling, Nutrition and Health Care (COUNSENUTH) P. O. Box 8218, Dar es Salaam. Kwa kushirikiana na: Halmashauri ya Manispaa ya Ilala S. L. P 20950, Dar es Salaam. Kimefadhiliwa na: Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Sehemu yoyote ya kijitabu hiki inaweza kunakiliwa kwa ajili ya matumizi yasiyo ya kibiashara ilimradi ionyeshwe kwamba taarifa hizo zimetoka kwenye kijitabu hiki. COUNSENUTH Information Series No.7 ii

YALIYOMO Shukrani......................... iv Utangulizi........................ 1 Mlo kamili....................... 2 Vidokezo vya kuzingatia katika kununua na kuhifadhi chakula Mboga-mboga................. 5 Matunda..................... 6 Samaki....................... 7 Mayai........................ 8 Nyama....................... 9 Maziwa...................... 10 Nafaka....................... 11 Kula nje ya nyumbani.............. 12 Tumia kwa kiasi................... 14 Ikiwezekana acha................... 15 Usalama wa chakula................ 16 Hitimisho........................ 18 Rejea............................ 19 Orodha ya vijitabu vingine........... 20 iii

SHUKRANI Kituo cha Ushauri Nasaha, Lishe na Afya (COUNSENUTH) kinatoa shukrani kwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kufadhili utayarishaji na uchapishaji wa kijitabu hiki. Shukrani za pekee kwa kamati ya UKIMWI ya Manispaa ya Ilala, Mwenyekiti - Diwani Mussa Azzan (Naibu Meya) na Mganga mkuu wa Manispaa ya Ilala - Dr. Judith Kahama kwa mchango wao katika kuboresha kijitabu hiki. Shukrani pia kwa SHDEPHA+, TAHEA na watu binafsi walioshiriki kwa njia mbalimbali katika kukamilisha kazi hii. iv

UTANGULIZI Binadamu wote wanahitaji chakula mchanganyiko na cha kutosha ili kuwa na hali bora ya afya na lishe. Hali bora ya lishe ni muhimu sana kwa watu wote hususan wale wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Hali bora ya lishe kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI husaidia kuboresha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali. Vilevile husaidia kurefusha kipindi mtu anachoishi tangu kupata uambukizo wa virusi vya UKIMWI hadi kuugua UKIMWI. Hali bora ya lishe huweza pia kupunguza makali ya magonjwa nyemelezi, husaidia dawa kufanya kazi vizuri mwilini na huboresha hali ya maisha kwa ujumla. Kijitabu hiki kina maelezo kuhusu ulaji bora, vidokezo muhimu katika ununuzi wa vyakula, hifadhi, mambo ya kuzingatia inapobidi kula nje ya nyumbani, usalama wa chakula na mengineyo. Maelezo yaliyomo ndani ya kijitabu hiki yanaweza kutumiwa na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, wale wanaowahudumia na jamii kwa ujumla. Kijitabu hiki kimetayarishwa mahsusi kwa watu wanaoishi Manispaa ya Ilala, vilevile kinaweza kutumiwa na watu wengine wanaoishi kwenye mazingira yanayohitaji kununua chakula au kula nje ya nyumbani. Jamii kwa ujumla pia inaweza kufaidika na maelezo ya kijitabu hiki. Ikumbukwe kuwa, kijitabu hiki kimetoa sehemu tu ya maelezo yanayohusu lishe na ulaji bora kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Kwa maelezo zaidi ni vizuri pia kusoma vijitabu vilivyoorodheshwa mwisho wa kijitabu hiki. 1

MLO KAMILI Mlo kamili huwa na chakula mchanganyiko na cha kutosha. Mlo huo unatakiwa kuwa na chakula angalau kimoja kutoka katika makundi yafuatayo ya vyakula na viliwe pamoja:- 1. Nafaka, mizizi na ndizi Vyakula hivi huchukua sehemu kubwa ya mlo na kwa kawaida ndivyo vyakula vikuu. Kundi hili hushirikisha mahindi, ulezi, mchele, ngano, mtama, uwele, viazi vikuu, viazi vitamu, viazi mviringo, mihogo, magimbi, ndizi, n.k. 2. Vyakula vya mikunde na vyenye asili ya wanyama Vyakula vilivyoko kwenye kundi hili ni pamoja na kunde, njegere, maharagwe, njugu mawe, fiwi, soya, karanga, dengu, choroko, aina zote za nyama, mayai, maziwa, dagaa, samaki, jibini, na wadudu wanaoliwa kama kumbikumbi, senene, n.k. 3. Mboga-mboga Kundi hili lina aina zote za mboga za majani kama matembele, mchicha, majani ya maboga, majani ya kunde, kisamvu, mgagani, figiri, spinachi, sukuma wiki, mnafu, mchunga, pia mboga nyingine kama karoti, biringanya bamia, maboga, matango, pilipili hoho, mlonge, nyanya chungu, mlenda, bitiruti na mboga mbalimbali za asili. 4. Matunda Kundi hili lina matunda aina zote kama pera, chungwa, embe, papai, karakara (pesheni), limau, ndimu, 2

chenza, parachichi, ndizi mbivu, zambarau, nanasi, fenesi, stafeli, pichesi, topetope, n.k. Pia yale matunda yanayoliwa ambayo hayalimwi na wakati mwingine huitwa matunda pori, ubora wake ni sawa na matunda mengine. Matunda hayo ni kama ukwaju, ubuyu, mabungo, embe ng ong o, mavilu, mikoche n.k. 5. Mafuta na Sukari Mafuta na sukari ni muhimu mwilini lakini vinahitajika vitumike kwa kiasi kidogo. Mafuta yanaweza kutokana na mimea kama nazi, mawese, mbegu zitoazo mafuta kama karanga, korosho, alizeti, ufuta, mbegu za maboga, kweme, na pia yale mafuta yatokanayo na wanyama kama siagi na samli. Sukari ni pamoja na miwa, asali, sukari, n.k. Maji Japo maji sio kundi la chakula lakini ni sehemu muhimu ya mlo. Maji ni muhimu kwa kurekebisha joto la mwili na kusaidia mfumo wa chakula. Ni muhimu kunywa maji angalau lita 1.5 (glasi 8) kwa siku. Maji huweza kutokana na kunywa maji safi na salama, madafu, maji ya matunda au maji yaliyochemshwa na viungo, n.k. KUMBUKA Mboga-mboga na matunda ni muhimu sana kuwepo katika kila mlo. Mara nyingi jamii zetu husahau mboga mboga na matunda. 3

VIDOKEZO VYA KUZINGATIA KATIKA KUNUNUA NA KUHIFADHI CHAKULA Mambo ya kuzingatia katika kununua chakula: Kuishi na virusi vya UKIMWI kunahitaji uangalifu zaidi na kujali ubora wa chakula kila wakati chakula kinaponunuliwa. Ili kuepuka ununuaji holela na usio wa muhimu au lazima, mnunuzi wa chakula anahitaji kuzingatia yafuatayo: Kufahamu kiasi cha pesa kilichopo kwa manunuzi ya vyakula; Kutayarisha orodha ya mahitaji muhimu ya chakula, inayoendana na kiasi cha pesa kilichopo; Kuorodhesha mahitaji muhimu ya familia hasa kwa watoto na wagonjwa; Uwezo na vifaa alivyonavyo kwa ajili ya kuhifadhi vyakula kwa mfano jokofu; Vyakula vilivyoko kwenye msimu kwani mara nyingi huwa na bei nafuu; Vyakula vyenye thamani zaidi kilishe mfano matunda halisi badala ya juisi au vinywaji bandia; Kununua zaidi vyakula freshi kuliko vilivyosindikwa kwani mara nyingi ni bora zaidi na ni bei nafuu; Kusoma maelezo (lebo) pale inapobidi kununua vyakula vilivyosindikwa; Vyakula vinavyoharibika upesi visinunuliwe kwa wingi. 4

Si vyema kwenda kununua chakula wakati una njaa kwani mara nyingi utajikuta unanunua vyakula ambavyo sio muhimu Ununuzi na uhifadhi wa baadhi ya vyakula: Mboga-mboga Ni muhimu kuwa waangalifu wakati wa kununua mboga-mboga kwa kuzingatia yafuatayo: Kuepuka mboga-mboga zote zenye michubuko, zilizonyauka, kupukutisha baadhi ya majani au zilizoharibika. Kuhakikisha mboga za majani ni kavu (hazina unyevu mwingi) na zina rangi ya asili. Kuepuka mboga-mboga zilizoliwa na wadudu, zilizoota ukungu au zilizoanza kuoza. Kwa mboga za mizizi kama karoti, kuhakikisha hakuna mikato, mikwaruzo yoyote au dalili ya kuanza kuota au kuoza. Kununua mboga-mboga kiasi cha kutosha matumizi ya muda mfupi. Mboga-mboga zote zihifadhiwe vizuri ili zisipoteze ubora. Mboga za majani hupoteza baadhi ya virutubishi na maji kwa urahisi wakati wa kuhifadhiwa, hivyo inapowezekana ni vyema kununua mboga-mboga kiasi kwa ajili ya matumizi ya muda mfupi. Yafuatayo ni muhimu: Ikibidi kuhifadhi kwa muda mfupi (kama siku moja), baada ya kuoshwa na maji kukauka, mboga-mboga (kama za majani, hoho, biringanya, bamia, matango) 5

ziwekwe kwenye mfuko laini, safi wa plastiki, kwenye sehemu yenye ubaridi, iliyo kavu na isiyo na mwanga. Mboga aina ya mizizi kama karoti, bitiruti n.k. zihifadhiwe sehemu ya wazi, iliyo kavu na inayoruhusu mzunguko wa hewa. Katika jokofu mboga-mboga zihifadhiwe sehemu isiyo na baridi kali. (Majokofu mengi huelekeza sehemu inayofaa kwa mboga-mboga). MUHIMU KWA KUDUMISHA UBORA WA MBOGA-MBOGA Osha kabla ya kukata; Katakata na kupika mara moja; Mboga-mboga zitayarishwe wakati ule wa kupika na zipikwe na maji kidogo. Kufanya hivyo kunapunguza upotevu wa baadhi ya virutubishi; Tumia mafuta kidogo katika mapishi; Pika kwa muda mfupi (ipua mara zinapoiva); Ziliwe mara tu baada ya kupikwa. Matunda Ununuzi wa matunda unapofanyika, ni muhimu kuzingatia yafuatayo: Kuhakikisha tunda limeiva vizuri, halina michubuko yoyote na halina dalili za kuoza. Kununua matunda yaliyo katika msimu kwani huwa na bei nafuu. Matunda pia yanahitaji uangalifu katika kuhifadhi. Hakikisha 6

kwamba: Matunda hayapati michubuko wakati wa kuhifadhi; Matunda yahifadhiwe mahali penye ubaridi na panaporuhusu mzunguko wa hewa; Matunda laini yatumike mapema au yahifadhiwe ndani ya jokofu kwani huweza kuharibika kwa urahisi zaidi. Iwapo hakuna jokofu ni vyema kununua matunda ya kutumia kwa muda mfupi. Samaki Unaponunua samaki wabichi zingatia yafuatayo: Samaki awe na harufu halisi ya samaki na si harufu tofauti au inayoashiria kuharibika; Awe na macho angavu na yaliyochomoza au kujitokeza kwa nje; Awe na mashavu au matamvua safi yaani rangi ya damu na si weusi; Awe na mkia uliokakamaa na awe mgumu au mkakamavu (stiff); Unapombonyeza kwa kidole au mkono na kuondoa pasibaki bonde; Awe na ngozi yenye unyevu; Kwa samaki wenye magamba hakikisha magamba yameshikana na ngozi; Inapowezekana samaki wabichi wanunuliwe na kupikwa kwa matumizi ya muda mfupi. Inapobidi kuhifadhi samaki wabichi yafuatayo ni muhimu: 7

Waondolewe uchafu wote, wasafishwe vizuri na wawekwe kwenye mfuko wa plastiki na kuhifadhiwa kwenye jokofu, sehemu yenye baridi kali au barafu (freezer); Samaki wabichi wasigusishwe na vyakula vingine hasa vile vinavyoliwa bila kupikwa, kwani wanaweza kuwa na vimelea vya magonjwa; Ndani ya jokofu samaki wawekwe mbali na vyakula vinavyofyonza harufu kwa urahisi, kama maziwa, juisi n.k. Mayai Ni muhimu kuzingatia yafuatayo wakati wa kununua mayai: Yai liwe na uzito fulani kwa hisia linaposhikwa (lisiwe jepesi kuliko umbile linavyoonekana); Hakikisha yai linapotazamwa kwa angani kwenye mwanga halionyeshi weusi wowote; Ikibidi yai linaweza kujaribiwa kama ni zima kwa kuliweka ndani ya chombo chenye maji yenye chumvi kidogo. Yai bovu huelea kwenye maji; Usinunue yai lililo na ufa. Hifadhi bora ya mayai ni muhimu kwani mayai yanaweza kuwa zalio zuri la vimelea vya maradhi. Yafuatayo ni muhimu: Inashauriwa kuhifadhi mayai mahali safi; Hakikisha sehemu ya yai iliyo bapa inaangalia juu ili kuepuka yai kuharibika mapema; 8

Inashauriwa kutoosha mayai wakati wa kuhifadhi, inapobidi yafutwe kwa kitambaa kikavu ili kuondoa vumbi. Yai likioshwa hupoteza ngozi fulani ya asili ambayo hulinda yai. Epuka kutumia yai lililo na ufa. Kwa wale wenye jokofu, mayai yahifadhiwe mahali penye ubaridi mdogo (majokofu mengi huonyesha sehemu ya kuweka mayai). Nyama Wakati wa kununua nyama mbichi zingatia yafuatayo: Nyama iwe na rangi halisi ya nyama freshi, mfano; nyama ya ng ombe iwe na rangi nyekundu; Hakikisha nyama ina harufu halisi ya nyama mbichi sio harufu inayoashiria kuharibika; Nyama iwe angavu na isidondoshe majimaji wala damu; Nyama isiwe na mifupa mingi; Epuka nyama yenye mafuta yanayoonekana kwa macho; Katika mazingira yetu ni bora kununua nyama mapema asubuhi kuliko mchana ambapo nyama huwa imeshinda dukani bila kuwekwa katika jokofu; Hakikisha nyama za ndani kwa mfano maini, figo, moyo, utumbo n.k. ni freshi na hazijaanza kuoza, nyama hizo zipikwe mapema baada ya kununuliwa. 9

KUMBUKA Kuosha nyama kabla ya kuikatakata; Kukatakata nyama kabla ya kupika husaidia nyama kuiva haraka; Kupika nyama pamoja na kiasi kidogo cha papai bichi lililopondwa, ndimu au limau husaidia nyama kulainika na kubaki na unyevu wake; Nyama iliyotolewa kwenye barafu na kuyeyushwa, isigandishwe tena. Uhifadhi bora wa nyama mbichi ni muhimu sana kwani nyama mbichi huweza kuwa zalio zuri la vimelea vya magonjwa. Ni vyema nyama mbichi ikanunuliwa kadiri ya mahitaji ya muda mfupi au ikahifadhiwa kwa kuzingatia yafuatayo: Nyama isafishwe kabla ya kuikata; Inapohifadhiwa iwekwe kwenye chombo cha plastiki chenye mfuniko au mfuko wa nailoni, kifurushi cha kutumia mara moja; Ihifadhiwe kwenye jokofu sehemu yenye baridi kali au barafu (freezer); Nyama iliyoganda ikiyeyushwa isigandishwe tena. Maziwa Maziwa yanayonunuliwa kwa wafugaji au ya kupima, yachemshwe vizuri pia yale yanayotumika kutengeneza mtindi. Kwa kawaida maziwa ya paketi (ya kiwandani) huwa yamechemshwa ili kuua vijidudu (Pasteuralized). Maziwa haya ni salama kwa kutumia. Unaponunua maziwa yaliyo kwenye paketi ni muhimu kuhakikisha kwamba paketi haijatoboka na muda wa kutumia haujamalizika. Inashauriwa: Maziwa freshi au mtindi yahifadhiwe kwenye jokofu, au yanunuliwe kiasi cha 10

kutumia kwa muda mfupi. Maziwa yaliyo kwenye paketi zinazoeleza kwamba yanaishi muda mrefu (UHT) yanaweza kuhifadhiwa katika joto la kawaida kama paketi haijafunguliwa. Ikishafunguliwa, yatumiwe mara moja au yawekwe kwenye jokofu, na tarehe za matumizi zilizoshauriwa zifuatwe. Nafaka Ni muhimu wakati wa kununua nafaka kama mahindi, mchele, ngano, ulezi, mtama na unga unaotokana na nafaka hizo kuhakikisha kwamba hazikuota ukungu, hazijawa na wadudu na hazina harufu ambayo sio ya kawaida. Kwa zile nafaka zilizofungwa kwenye paketi, hakikisha tarehe ya kutumia haijamalizika. Nafaka zihifadhiwe mahali pakavu. Vyakula vingine Hakikisha unga, mihogo, karanga havina ukungu vinaponunuliwa na vihifadhiwe mahali pakavu. VIDOKEZO KUHUSU MATUMIZI YA JOKOFU Chakula kiwekwe kwenye chombo au kifurushi kwa matumizi ya mara moja; Chakula kilichotolewa kwenye jokofu kichemshwe kabisa kabla ya kuliwa; Nyama mbichi au samaki wabichi wawekwe sehemu yenye baridi kali (freezer), katika vifurushi vya matumizi ya mara moja; Nyama au samaki iliyotolewa katika barafu ikiyeyushwa ipikwe yote, isigandishwe tena; Hakikisha nyama mbichi au samaki wabichi havigusishwi na vyakula vingine. 11

Hii huepusha uambukizo unaoweza kutokana na vyakula hivi; Matunda yaliyokatwakatwa yawekwe kwenye chombo chenye mfuniko, na yahifadhiwe kwa muda mfupi; Vyakula ndani ya jokofu vifunikwe au kufungwa kwenye mfuko safi wa plastiki ili kudumisha ubora wake na kuepuka muingiliano wa harufu; Maji ya kunywa yafunikwe; Mlango wa jokofu usiachwe wazi kwa muda mrefu. Funga mara unapotoa au kuweka kitu. KULA NJE YA NYUMBANI Zipo sababu nyingi zinazomfanya mtu kula nje ya nyumbani au katika mazingira ambayo mara nyingi mlaji hana uwezo wa kudhibiti namna chakula kinavyopikwa au vitu vilivyochanganywa ndani yake. Ni muhimu kwa mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI kuwa mwangalifu zaidi kwani chakula kinaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa iwapo hakitatayarishwa katika hali ya usafi na usalama. Sehemu ambazo mara nyingi mtu anakula nje ya nyumbani ni pamoja na:- Hotelini au katika migahawa; Kafeteria; Katika sherehe au misiba; Vyakula vinavyouzwa kando ya barabara; Wauzaji wanaotembeza chakula n.k. Kisheria sehemu zote zinazouza chakula zinatakiwa kuzingatia usafi na usalama, lakini inawezekana sio sehemu zote zinatimiza masharti ya usafi. Hivyo ni muhimu sana kuwa 12

waangalifu hasa kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwani kinga yao ya mwili imepungua. Mambo ya kuzingatia wakati wa kula nje ya nyumbani: Kuepuka mboga-mboga mbichi kama kachumbari na saladi, kwani zina hatari kubwa zaidi ya kuwa na vimelea vya magonjwa, iwapo hazikutayarishwa katika hali ya usafi; Kama ni hoteli uliza kama inawezekana kutengenezewa chakula namna unavyotaka; Kuhakikisha nyama, samaki, mayai ni vya moto na vimeiva vizuri; Vyakula vinavyopikwa kwa wingi na kuachwa kusubiri wateja kwa muda mrefu vinaweza kuwa sio salama, ni bora kuviepuka; Vyakula vinavyouzwa kando ya barabara mara nyingi uhifadhi wake sio salama, hivyo ni bora kuviepuka kwani hatari ya sibiko (contamination) ni kubwa; Mara nyingi vyakula vinavyopikwa katika mikusanyiko kama misiba au sherehe huwa ni vingi. Inawezekana kukatokea upungufu wa vifaa au mahitaji mengine, na hivyo kusababisha sibiko (contamination) katika chakula. Ni vizuri mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI kuwa mwangalifu hasa inapobidi kula katika mikusanyiko ya watu. Ni vyema kuepuka pale inapowezekana. 13

TUMIA KWA KIASI!!! Baadhi ya vyakula huhitajika mwilini kwa kiasi kidogo. Ni muhimu kutumia vyakula hivi kwa kiasi. Vyakula hivyo ni kama; mafuta, sukari na chumvi. Mafuta Mafuta huhitajika mwilini kwa kiasi. Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anatakiwa kutumia mafuta, ila atumie kwa kiasi. Ikumbukwe kwamba vyakula vinavyopikwa kwa kukaangwa au kutumbukizwa kwenye mafuta na vile vinavyokandwa kwa mafuta au tui la nazi huwa na mafuta mengi. Vyakula hivi vitumike kwa kiasi. Mfano wa vyakula hivyo ni kama maandazi, chapati, chipsi, vitumbua, sambusa, kababu, kaukau, crisps, n.k. Vyakula vingine vinavyoweza kuwa na mafuta mengi ni pamoja na soseji, aiskrimu za maziwa, baadhi ya biskuti na mbegu zitoazo mafuta. Badala ya kupikwa kwa kutumbukiza kwenye mafuta njia nyingine za kupika zinaweza kutumika ili kupunguza mafuta kwa mfano; kuoka, kuchoma, kupika kwa mvuke au kuchemsha. Pia ni vizuri kuondoa mafuta yanayoonekana kwa macho kwenye nyama kabla ya kupika. Ni bora zaidi kutumia mafuta yanayotokana na mimea lakini pale yanapokosekana, mafuta yanayotokana na wanyama yanaweza kutumika. Usiache kabisa kutumia mafuta. Sukari Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anahitaji sukari kwa sababu inampatia nguvu. Hata hivyo vipo vyakula vingine ambavyo 14

humpatia mtu nguvu, hivyo vyakula vyenye sukari kwa wingi vitumike kwa kiasi. Vyakula hivyo ni pamoja na sukari, sukari guru, keki, chokoleti, jamu, soda na vinywaji vingine vyenye sukari kwa wingi. Ni vyema vyakula hivi vitumike mara chache au kwa kiasi. Chumvi Chumvi huongeza ladha kwenye chakula na huupatia mwili baadhi ya madini. Wakati mwingine chumvi hutumika katika kuhifadhi vyakula. Chumvi nyingi sio nzuri kwa afya. Vyakula vyenye chumvi nyingi ni pamoja na vyakula vilivyosindikwa kwa chumvi kama nguru aliyekaushwa, soseji, achari, baadhi ya vyakula vilivyosindikwa kama samaki na nyama za makopo, supu za paketi, baadhi ya vyakula vingine vya makopo, bacon n.k. Vyakula hivi vinapotumika vitumike kwa kiasi. Ili kupunguza matumizi ya chumvi nyingi, kiasi kidogo cha chumvi kitumike katika kupikia chakula na ni vizuri kuepuka kuongeza chumvi mezani. IKIWEZEKANA ACHA!!! Baadhi ya vyakula havina umuhimu mwilini kwa mfano pombe au vinywaji vyenye kafeini kwa wingi. Ni vizuri kupunguza matumizi ya vyakula hivi au kuviacha kabisa. Pombe Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anashauriwa kupunguza sana matumizi ya pombe na ikiwezekana kuacha kabisa. Matumizi ya pombe yameonyesha madhara mbalimbali katika mwili kwa kuingilia ulaji wa chakula, uyeyushwaji wa chakula, ufyonzwaji 15

wa virutubishi mwilini pamoja na uwekaji akiba wa baadhi ya virutubishi. Pia imeonekana kwamba pombe huongeza hatari ya kupata magonjwa sugu kama saratani hasa za kinywa, koromeo, zoroto (larynx) na ini. Vilevile huongeza hatari ya kupata vidonda vya tumbo na magonjwa ya moyo. Vinywaji vyenye kileo ni pamoja na bia, mvinyo, pombe zote kali, pombe za kienyeji n.k. Ni vyema kujaribu kutumia vinywaji visivyo na kileo kama juisi ya matunda halisi, madafu, togwa n.k. Kafeini Kafeini hupatikana kwenye baadhi ya vinywaji na vyakula. Kafeini ni kichangamsha mwili, lakini huzuia usharabu wa madini ya chuma yatokanayo na vyakula vya mimea. Vyakula vyenye kafeini kwa wingi ni pamoja na chai, kahawa, baadhi ya soda, chokoleti na kokoa. Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anashauriwa kupunguza matumizi ya vinywaji hivi. Inapobidi kutumia vinywaji hivi, vitumike kwa kiasi kidogo, na vitumike angalau saa moja kabla au baada ya kula. Ni vizuri kujaribu vinywaji vya aina nyingine, kwa mfano vile vinavyotengenezwa kutokana na viungo, majani ya mchaichai, majani ya mlimau, choya (rozela), nanaa, tangawizi na vinginevyo, au juisi itokanayo na matunda halisi. USALAMA WA CHAKULA Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI yuko kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali kwa urahisi zaidi. Hivyo basi ni muhimu kwa mtu huyo au mtayarishaji wa chakula kuzingatia yafuatayo ili kufanya 16

chakula na maji viwe safi na salama kwa mtumiaji: Vyombo vinavyotumika kutayarishia na kupakulia chakula viwe safi. Vyombo na vifaa vilivyotumika kutayarisha nyama mbichi, samaki wabichi na mayai mabichi vioshwe vizuri kwa maji na sabuni kabla ya kuvitumia kwa matumizi mengine. Majivu yanaweza kutumika pale ambapo hakuna sabuni. Kuhakikisha chakula kimepikwa na kuiva vyema, na pia kiliwe kingali cha moto. Kuosha matunda na mboga-mboga kwa maji ya kutosha. Mboga zinazoliwa bila kupikwa mfano kachumbari na matunda yanayoliwa na maganda yasafishwe kwa maji salama. Sehemu zenye michubuko katika mboga na matunda zikatwe na kutupwa. Kuepuka nafaka au vyakula vilivyoota ukungu. Kuhakikisha kuwa nyama, samaki na mayai vinapikwa na kuiva vizuri ili kuepuka maambukizo ya magonjwa. Vyakula hivi kamwe visiliwe vikiwa vibichi. Kuepuka vyakula vilivyokaa zaidi ya saa mbili baada ya kupikwa au viporo, ikibidi kuliwa vichemshwe vizuri kabla ya kuliwa hata kama bado vina uvuguvugu. Ni bora kuepuka viporo. Kuepuka mgusano wa vyakula vibichi na vile vilivyopikwa, hasa nyama mbichi, samaki wabichi na mayai mabichi. Kuchemsha maji ya kunywa na kuyaacha yaendelee kuchemka kwa muda wa dakika 17

5 hadi 10. Maji hayo yatunzwe katika chombo safi chenye mfuniko. Iwapo unahitaji kutumia barafu, hakikisha maji yaliyotumika kutengenezea barafu yalichemshwa. Kuosha mikono kwa sabuni na maji ya kutosha kabla ya kutayarisha chakula. Majivu yanaweza kutumika pale ambapo hakuna sabuni. Kunawa mikono mara baada ya kutumia choo au kujisaidia, kupiga chafya, kufuta kamasi au kushika taka. Kuzingatia usafi wa mwili na nguo. Kufunga vidonda vya mkononi ili kuzuia sibiko (contamination) wakati wa kutayarisha chakula. Sehemu zote za kutayarishia chakula ziwe safi. Funika vyakula na maji kwa vyombo safi kuzuia wadudu hasa inzi. KUMBUKA Inapobidi kula nje ya nyumbani, ni muhimu kuhakikisha unakula chakula cha moto. Chakula ambacho hakikupikwa nyumbani kwako inaweza kuwa vigumu kujua usafi na usalama wake. Inapowezekana, jaribu kula mahali ambapo unaweza kudhibiti usafi na usalama wa chakula na maji. HITIMISHO Hali bora ya lishe ni muhimu katika kuboresha afya ya mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI. Ikumbukwe kwamba ulaji bora ni pamoja na kuzingatia ununuzi bora wa vyakula 18

mbalimbali, uhifadhi bora, usafi na usalama. Mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI anashauriwa kutumia vizuri kiasi cha pesa kilichopo katika kununua vyakula ambavyo vina thamani kubwa kilishe na vinavyoupatia mwili virutubishi muhimu. Sio lazima kwamba vyakula vyenye bei kubwa ndio bora zaidi. Vyakula vingi vya asili ambavyo sio vya bei kubwa sana ni bora pia kilishe. Ikumbukwe kuwa mtu anayeishi na virusi vya UKIMWI inabidi awe mwangalifu zaidi katika usafi na usalama wa chakula, kwani kinga ya mwili imepungua hivyo anaweza kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali kwa urahisi zaidi. REJEA 1. Burgess, A. and others, Community Nutrition for Eastern Africa, African Medical and Research Foundation, Nairobi, Kenya, (1994). 2. FAO - Living well with HIV/AIDS, A manual on nutritional care and support for people living with HIV, (2002). 3. FAO - Get the best from your food (1997) 4. Ndungi, H.K., Food and Nutrition for Schools and Colleges, Nairobi, (1992). 5. NFTRC, Healthy eating, shopping for food and food safety guidelines, (Botswana). 6. Tull, A., Food and Nutrition, GCSE Edition, Oxford University Press, (1991). 19

Orodha ya vijitabu vingine kuhusu Lishe na Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI vilivyotolewa na COUNSENUTH 1. Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI: Vidokezo Muhimu (COUNSENUTH, Information series No. 2), Toleo la Pili, January, 2004. 2. Lishe na Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI: Majibu ya Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara (COUNSENUTH, Information series No. 3) Toleo la Pili, January, 2004. 3. Lishe na Ulaji Bora kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI: Vyakula Vinavyoboresha Uyeyushwaji wa Chakula na Ufyonzwaji wa Virutubishi Mwilini (COUNSENUTH Information series No. 4), March, 2003. 4. Ulishaji wa Mtoto Mchanga kwa Mama Mwenye Virusi vya UKIMWI: Vidokezo Muhimu kwa Washauri Nasaha (COUNSENUTH Information series No. 1), Toleo la Pili, January, 2004. 5. Matumizi ya Viungo vya Vyakula katika Kuboresha Lishe na Afya (COUNSENUTH, Information series No. 6), Toleo la Kwanza, March, 2004. 20

Kijarida hiki kimetayarishwa na: The Centre for Counselling, Nutrition and Health Care (COUNSENUTH) United Nations Rd./Kilombero Str. Plot No. 432, Flat No. 3 P. O. Box 8218, Dar es Salaam, Tanzania Tel/Fax: +255 22 2152705, Cell: 0744 279145 Kwa maelezo zaidi wasiliana na: Mkurugenzi The Centre for Counselling, Nutrition and Health Care (COUNSENUTH) Kwa kushirikiana na: Halmashauri ya Manispaa ya Ilala S.L.P 20950 Dar es Salaam Kimefadhiliwa na : Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Reprinting facilitated by COUNSENUTH and MUCHS, in partnership with the Government of Tanzania. Designed & printed by: Desktop Productions Limited P.O. Box 20936, Dar es Salaam, Tanzania Contact: 0748 387899, Email: sales@dtptz.com Reprinted January 2005 25