Mhashamu Askofu Jude Thaddaeus Ruwa ichi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; Mwadhama Policarp Kardinali Pengo,

Similar documents
wasiofaa. Naomba sana kila raia afanye bidii awezavyo kumkaribia Mwenyezi Mungu vile anavyoona inafaa, lakini asipitishe hukumu juu ya wengine.

MAADHIMISHO YA MIAKA 15 YA FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY

Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame M. Mbarawa (Mb.); Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge wote mliohudhuria;

Dodoma ambako kikao cha Bunge kinaendelea kuja kushiriki japo sehemu ya uzinduzi wa mkutano.

Azimio la Umoja wa Mataifa Kuhusu Watetezi wa Haki za Binadamu

Information for assessors (do not distribute this page to participants):

5. Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilijadili kwa kina Miswada ifuatayo:

TAARIFA FUPI KUHUSU SERA YA TAIFA YA ELIMU

Elimu ya Msingi inaelekea Upande Sahihi? Kufikiri na Nyerere Rakesh Rajani

JAMHURI YA KENYA. Mkakati wa Ushirikiano MUKHTASARI FY Public Disclosure Authorized. Public Disclosure Authorized

GOVERNMENT NOTICE No... PUBLISHED ON THE ELECTRICITY ACT, (CAP.131) ORDER. (Made under Section 23)

HOTUBA YA WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU: KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU MHE

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA,KWA WANANCHI, 30 SEPTEMBA, 2001

Human Rights Are Universal And Yet...

Azimio lililopitishwa na Mkutano Mkuu tarehe 18 Desemba 2013 [juu ya taarifa ya Kamati ya Tatu (A/68/456/Add.2)]

JUA HAKI ZAKO, SEHEMU YA 1

Agano Lililofunikwa Kwa Damu

UTANGULIZI ANUANI NA MANDHARI YA CHUO

UNIVERSITY OF CAMBRIDGE INTERNATIONAL EXAMINATIONS General Certificate of Education Ordinary Level. SWAHILI 3162/01 Paper 1 May/June 2013

United Pentecostal Church June 2017

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO

Pronunciation: Mä-hret Zäläke Ndal-ka-tscho Molla Mare Gebre-gzabiär 1/12

PDF created with pdffactory trial version

TAFSIRI RAHISI YA MPANGO WA MAENDELEO YA AFYA YA MSINGI (MMAM)

GOVERNMENT NOTICE No... PUBLISHED ON THE ELECTRICITY ACT, (CAP.131) ORDER. (Made under Section 23)

Shabaha ya Mazungumzo haya

Theolojia Ujumla. Mike Taylor Semester Munguishi Bible College

MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI 2001

Haja Ya Dini. Author(s): Publisher(s): Translator(s): Category: Topic Tags: Featured Category: Published on Al-Islam.org (

MAPENDEKEZO YA MTANDAO WA WANAWAKE NA KATIBA TANZANIA

Songa kwenye kilele cha upeo. Masuala ya Msingi na Ujuzi juu ya Uendeshaji wa Serikali za Mitaa

SERA & TARATIBU YA YALE NEW HAVEN HEALTH

KITEGO CHA MAREKEBISHO NA HAKI ZA MTOTO

Ripoti ya Mwaka ya Utekelezaji wa MKUKUTA 2006/07

TANZANIA OSAKA ALUMNI. Kitabu cha Mbinu Bora

Ellen White, waasisi wa Kiadventista,na Sabato Lunar

Dibaji ya Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya Uongozi

Elimukombozi, Lugha na Upashanaji Habari nchini Tanzania, katika Muktadha wa Utandawazi

MUNGU ANADHIHIRISHWA KUPITIA KWA YESU KRISTO.

BUNGE LA TANZANIA MAJADILIANO YA BUNGE MKUTANO WA SABA. Kikao cha Thelathini na Tisa Tarehe 1 Juni, (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A

MAKUBALIANO YA 2005 YA ULINZI NA UKUZAJI WA VIELELEZO VYA TAMADUNI ANUWAI

Mukhtasari Wa Mabishano Kwa Na Dhidi Ya Vikombe Vingi Vya Ushirika

TAMKO LA JUKWAA LA HAKI ZA WATOTO (TCRF) KUHUSU HAKI ZA WATOTO KATIKA KATIBA MPYA

usudi la Maisha Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na kupishana usiku na mchana, kuna kweli ishara kwa wenye akili, ambaye mkumbuke-

"ATATOKEA MARA YA PILI, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu." Waebrania 9:28.

RIPOTI YA WARSHA KUHUSU HABARI KWA AJILI YA UWAJIBIKAJI

Misamaha ya kodi Tanzania: Je, ni mikubwa sana na kutufanya tuwe tegemezi kwa misaada?

ATHARI ZA MABADILIKO YA TABIANCHI KWA UCHUMI WA ZANZIBAR

Mwongozo kwa Lugha Rahisi wa Sera ya Maendeleo ya Ushirika na Sheria ya Vyama vya Ushirika Tanzania Bara

Kufafanua Upya Elimu Bora Tanzania: Kutoka Zana za Dufundishia mpaka Uwezo wa Wanafunzi 1 Oktoba 2007

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika,

KANISA NA UAMSHO Na Mchg. Dkt. Faith Lugazia

Kutetea Haki za Binadamu

WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI TAASISI YA ELIMU TANZANIA MTAALA WA ELIMU YA MSINGI TANZANIA

WEWE NI NANI? Toleo X Toleo Ukweli wa Injeli Toleo 23

Tumaini Kwa Afrika. Thomas Schirrmacher. Hoja 66. Dibaji na Prof. Mchungaji Dk. Thomas K. Johnson. Thomas Schirrmacher Tumaini Kwa Afrika TASCM RVB

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) Muhtasari Rakesh Rajani na George Omondi

Elimu Ina Umuhimu gani katika Jamii? Kuelekea Elimu Sahihi

LUGHA YA KISWAHILI KATIKA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA ELIMU SHULE ZA SEKONDARI

MKAKATI WA PILI WA TAIFA WA KUDHIBITI UKIMWI ( )

KUSHUKA KWA HADHI YA LUGHA ZA JAMII NCHINI TANZANIA YOHANA P. MSANJILA University of Dar es Salaam, Tanzania

Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA MAJADILIANO YA BUNGE MKUTANO WA KUMI NA TISA. Kikao cha Pili - Tarehe 14 Aprili, 2010

Ushindi ndani ya Kristo W. W. PRESCOTT

BUNGE LA TANZANIA MKUTANO WA NANE. Kikao cha Ishirini na Nane Tarehe 16 Julai, (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A

Mipango ya miradi katika udugu

Juni 3-9 Pata Manufaa Kamili kwakusomabiblia

Maisha Yaliyojaa Maombi

Ufunguo wa Kutaalamika Haraka

SautiElimu. Sauti Yako Isikike

Kiswahili, utandawazi na umoja wa Afrika

Summaries of GC Reports 2012, Vol. 2, Sec. 1, Swahili

Hati ya kuhitimu kisomo Kenya (K.C.S.E)

MKAKATI WA PILI WA TAIFA WA KUDHIBITI UKIMWI ( )

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA. Ifahamu Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo. TOLEO Na.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Ndugu na dada zangu wapendwa,

Vol. 113, Namba 1, 2013 ISSN

MIONGOZO MIWILI KUPAA NA KUTUNGULIWA KWA AZIMIO LA ARUSHA

Miradi na jamii. 3.1 Utangulizi

WAFUNAJI WA NAFSI ABC By Vagn Rasmussen Translation by Lydia Madsen

KAMATI ZA KUDHIBITI UKIMWI NCHINI TANZANIA

Mwongozo wa Utamaduni Toleo la Kwanza

UTARATIBU WA KANISA. 2 Jambo la kwanza ninalotaka kusema ni kwamba mchungaji. 3 Sisi tunaamini katika Kanisa la kimitume, tukifundisha

Nilikua na Ndoto ya Kumaliza Shule Changamoto za Elimu ya Sekondari Tanzania

GRACE COMMUNION INTERNATIONAL KANUNI YA IMANI

Ripoti Fupi ya Nchi kuhusu Kazi Zenye Staha TANZANIA (bara)

Kubadili Sheria Za Mbegu Na Ulinzi Wa Aina Za Mbegu Na Mimea Nchini Tanzania

Kocha Mkuu. mabingwa. itakuwa INASTAHILI. Ili Kutoa mafunzo kwa wanafunzi wako kuwa. itakuwa ya kuumiza. Itachukua muda. Itahitaji moyo wa kujitoa.

HISTORIA, MAENDELEO NA MABADILIKO YA KATIBA TANZANIA TANGU UHURU HADI MIAKA HAMSINI YA UHURU 9 DESEMBA 2011.

MACHAGUO YA UZAZI KUFIKIRIA KUWA MZAZI

3 FEBRUARI, 2015 BUNGE LA TANZANIA MAJADILIANO YA BUNGE MKUTANO WA KUMI NA NANE. Kikao cha Saba - Tarehe 3 Februari, 2015

BUNGE LA TANZANIA MAJADILIANO YA BUNGE MKUTANO WA KUMI NA MOJA. Kikao cha Hamsini na Tatu Tarehe 19 Juni, (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi)

Watumishi Wa Kristo. Ellis P. Forsman. Watumishi Wa Kristo (Servants Of Christ) 1

MKAKATI ATHARI YA MAZINGIRA NA KIJAMII YA KAZI YA PRO-ROUTES. Ombi kwa ajili ya fedha za umma wa mradi wa ziada

Kuwafikia waliotengwa

April 14, 2016 COUNTY ASSEMBLY DEBATES 52

Maisha Ya Mkristo Ni Nini?

walozaliwa, si kwa damu, wala mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, mbali kwa Mungu. Sisi sio tena binadamu wa kawaida tu kwa sababu sisi ni w

MIAKA 500 YA MATENGENEZO YA KANISA NA USHUHUDA WETU Na Askofu Dr. Abednego Keshomshahara

Transcription:

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU, KWENYE SHEREHE YA KUADHIMISHA MIAKA HAMSINI YA BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI TANZANIA, TAREHE 08 JUNI 2008, MSIMBAZI CENTRE, DAR ES SALAAM Mhashamu Askofu Jude Thaddaeus Ruwa ichi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania; Mwadhama Policarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam; Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth, Balozi wa Vatican, Tanzania; Wahashamu Maaskofu; Waheshimiwa Mapadri; Waheshimiwa Watawa; Viongozi wa Kanisa na Waumini; Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana. TUMSIFU YESU KRISTU!! Naungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukusanyika hapa leo katika sherehe hii ya Kuadhimisha Miaka 50 ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Hii ni siku ya furaha na siku njema iliyopangwa na Mungu kushuhudia uwepo wa Baraza hili tangu lianzishwe rasmi mapema mwaka 1956. Maandiko ya Mtunga Zaburi yanasema: Siku hii ndiyo aliyoifanya BWANA. Tutaishangilia na kufurahia (Zaburi 118:24). Aidha, nitumie nafasi hii kutambua wageni wote mliotoka nje na ndani ya Tanzania. Nasema: For our visitors from abroad, KARIBUNI SANA TANZANIA. You are welcome to Tanzania and feel at home!!

Wahashamu Maaskofu, nianze kwa kutoa salaam kutoka kwa Rais, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye awali alitarajia angeshiriki nanyi siku ya leo, lakini kutokana na majukumu mengine ya Kitaifa baada ya kumalizika kwa mkutano mkubwa wa Leon Sullivan, haikuwezekana kuwa nasi leo. Anawasalimu na anawapongeza kwa kutimiza miaka 50 ya Baraza hili. Aidha, anawatakia wote kheri na baraka katika majukumu yenu ya kuwaongoza wana kondoo wa Mungu katika nchi yetu. Nami nitumie fursa hii kuungana na Mheshimiwa Rais, kuwapongeza kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kipindi chote cha uhai wa Baraza hili. Nawapongeza kwa majukumu mazito ambayo Baraza limetekeleza. Hongereni Sana! Wahashamu Maaskofu, moja ya majukumu muhimu yaliyotekelezwa na Baraza hili ni kuliweka Kanisa katika hali ya Umoja na Mshikamano. Wote tunatambua na tunakubali kuwa viongozi wa dini, ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga mshikamano wa Kitaifa. Historia inaonyesha kwamba, wakati harakati za kupigania Uhuru zilianza miaka ya 1950, tayari viongozi wa dini ukiwemo Umoja wa Maaskofu Tanzania, walikuwa wamekwishaanza kujenga misingi ya muungano mapema tangu mwaka 1912. Huu ni uthibitisho kuwa harakati za kujenga Umoja zilianza zamani. Harakati hizo za upande wa siasa zilikwenda sambamba na harakati za upande wa Kidini kwa pamoja zikachangia kuwaleta wananchi kwa pamoja na hivyo kujenga umoja wa kitaifa. Wahashamu Maaskofu na Wageni Waalikwa, tunapoangalia mwanzo wa Umoja huu wa Maaskofu, tunabaini kwamba malengo yake hakika yaliangalia maendeleo ya mwananchi. Tumebaini hili katika jina la kwanza kabisa ambalo umoja huu ulijisajili Serikalini. kumbukumbu zinaonyesha kwamba, mwaka 1958, chombo hiki cha Maaskofu kilisajiliwa Serikalini kwa jina la Tanganyika Catholic Welfare Organization. Neno linalogusa maslahi ya jamii ndilo lililokuwa kiini cha umoja huu. Welfare! Jamii imejionea yenyewe kwamba hata baada ya jina kubadilika mwaka 1965 na kuwa Tanzania Episcopal Conference au Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, bado moyo na ile dhamira ya tangu mwanzo ya kumhudumia mwananchi imedumu. Mafanikio Wahashamu Maaskofu, katika kipindi hiki cha miaka 50, Baraza la Maaskofu Katoliki, limepata mafanikio mengi katika nyanja ya kiuchungaji na katika maendeleo ya jamii. Ninaelewa tangu mwanzo Baraza hili limekuwa kinara wa Maendeleo Fungamano ya Binadamu (Human Integral Development). Hili linathibitishwa na ukweli kwamba, idara za

mwanzo kabisa zilizoanzishwa katika Baraza la Maaskofu, zilikuwa zile zinazojishughulisha na mambo ya kijamii. Ziko idara za elimu, afya, maendeleo ya jamii (Caritas) na mawasiliano. Hizi ni idara zilizoanzishwa muda mrefu tangu mwaka 1956. Elimu Wahashamu Maaskofu na Wageni Waalikwa, madhehebu ya dini yamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza huduma za jamii nchini. Kwa mfano, katika upande wa elimu, Kanisa Katoliki limetoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu. Nakumbuka historia ya sekondari chache, kama vile Marian College ambayo kwa sasa ni Sekondari ya Kilakala au St. Francis ambayo sasa ni Sekondari ya Pugu. Hii ilijengwa mwaka 1957. Kuna Kurasini ambayo sasa ni Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) ilijengwa mwaka 1967. Ninazo taarifa kwamba Maaskofu Tanzania, mmoja mmoja na katika ujumla wao, sasa hivi wanamiliki shule 150 za sekondari, vyuo takriban 200 vya mafunzo stadi, Vyuo viwili vya walimu, Chuo Kikuu cha St. Augustine chenye vyuo vikuu vishiriki vitatu. Aidha, nimepata taarifa kwamba, mwaka huu wahitimu kutoka katika vyuo vikuu vya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watakuwa zaidi ya 5,000. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa mfano, nalo limechangia sana katika elimu. Kwa sasa lina shule za awali 469, shule za msingi maalumu kwa walemavu 10, shule za sekondari 61, vyuo vya elimu na ufundi 35, Chuo Kikuu na Vyuo Vikuu vishiriki sita. Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) limechangia kwa kuwa na shule za chekechea 500, shule za msingi tatu (3), shule za sekondari 27, Chuo cha Ualimu cha Al-Haramain na Chuo Kikuu cha Morogoro cha Kiislam kimoja. Haya ni maendeleo na mafanikio makubwa yanayowagusa wananchi moja kwa moja. Asanteni Sana. Afya Wahashamu Maaskofu, katika upande wa huduma za afya, historia inaonyesha kwamba mwaka 1961, Maaskofu mmoja mmoja na katika ujumla wao walikuwa wanamiliki Hospitali 23, Zahanati 74, Kliniki 64, Vituo 7 vya Wakoma na Vyuo 5 vya Wauguzi. Leo hii ziko Hospitali 44, Zahanati 328 na Vituo 52 vya Afya. KKKT wanazo Hospitali 138, Vituo vya Afya 13, Vituo vya Wauguzi sita (6), Vituo vya Watoto Yatima 11 na Kituo cha Wazee kimoja (1). Baraza Kuu la Waislam Tanzania limejenga Vituo vya Afya 12, Vituo vya kulelea Watoto Yatima sita (6) na Mradi wa Kitengo cha UKIMWI ambao uko makao makuu ya BAKWATA. Kwa kupitia vyombo hivi vya afya ambavyo vimesambaa Tanzania nzima, Baraza la Maaskofu linachangia asilimia 20 ya huduma za afya katika nchi yetu!! Tunawashukuru sana kwa mchango wenu! Vilevile, tunatambua mchango wa Baraza hili kwa kupitia vyombo vyake kama vile Caritas Tanzania vinavyofanya kazi kwa kusaidia wananchi wanaoathirika na majanga mbalimbali kama vile njaa, mafuriko, ukame, n.k. Kwa upande wa KKKT wanasaidia majanga mbalimbali kupitia Tanzania Commission for Refugees Services (TCRS), na Action by Churches Together (ACT), n.k. Mafanikio yote haya yamewezekana kwa vile madhehebu ya dini yakiongozwa na

ninyi viongozi kwa kuwashirikisha waumini wenu mlikuwa na nia thabiti ya kumkomboa Mtanzania kutoka katika adui ujinga, maradhi na umaskini. Tunajua pia kuwa, nia njema pekee bila raslimali watu na fedha, isingeweza kufanya hayo yote. Tunatambua kwa dhati mchango mkubwa wa Serikali ya Vatican na Makanisa mengine ulimwenguni. Tunawashukuru wote waliowaunga mkono Maaskofu wetu Tanzania katika nia yao njema ya kumkomboa Mtanzania. Thank you very much The Vatican for your assistance to the Government of Tanzania! Changamoto Wahashamu Maaskofu, tunazo changamoto kubwa bado zinazoikabili nchi yetu katika nyanja za elimu, afya, maji, watoto yatima, watoto wenye ulemavu, suala zima la janga la UKIMWI na suala la ushirikina. Changamoto hizi zinatupa vigezo vya kupima juhudi na uwezo wetu kama viongozi wa serikali na viongozi wa dini katika kuhudumia jamii. Ninachotaka kusema ni kwamba, tuna kazi kubwa katika kuilea Jamii katika kukabiliana na changamoto hizi. Sisi kama Serikali tunaweza kurekebisha mambo ya kimwili. Lakini ninyi kama wachungaji wa Kondoo wa BWANA, mnayo nafasi ya kubeba mzigo mkubwa wa wanakondoo Kiroho. Waumini wenye shida kama ya ulemavu na UKIMWI watahitaji upendo, uvumilivu na moyo wa kuwasaidia. Wanahitaji walindwe katika mazingira magumu yanayowakabili kwa sasa. Aidha, tunahitaji kuwaelekeza juu ya ufumbuzi wa shida zinazowakabili huku tukiwasihi wasikate tamaa kwa maana shida hazikuumbwa kwa ajili yao tu, bali binadamu yoyote. Uko msemo wa watu wa kale usemao: I wept because I had no shoes until I saw a man who had no feet ikimaanisha: Nililia sana kwa sababu sikuwa na viatu lakini nilikoma kulia nilipokutana na mtu ambaye hana mguu. Hivyo tunawakumbusha kuwa kutokana na udhaifu wetu kama binadamu wataweza kuwa wanasononeka kwa kukosa viatu wakati kuna wasio na miguu kabisa na hawajakata tamaa ya kuishi. Aidha, ni rahisi kuyakuza matatizo yaliyopo yakaonekana makubwa sana tukasahau Baraka ambayo Mungu wetu Mkuu ametupatia. Nasisitiza kuwa katika kazi ya kuwaongoza waumini wa kanisa au wananchi, jukumu kubwa ni kuwasaidia kupata ufumbuzi wa matatizo yao. Mauaji ya Maalbino

Wahashamu Maaskofu, Taifa letu kwa siku za hivi karibuni limekumbwa na tatizo la imani za kishirikina na kichawi. Napenda nichukue nafasi hii kulisema hili kwa uchungu na masikitiko makubwa sana. Sote kwa pamoja, Serikali, Madhehebu ya Dini na wananchi kwa ujumla, tumeshuhudia mauaji ya kutisha ya watu wasiokuwa na hatia kwa ajili ya imani za kujipatia utajiri wa haraka. Tumeshuhudia ndugu zetu Maalbino wakiuawa eti kwa sababu ya imani za kichawi kuwa viungo vyao vinaleta utajiri. Haya ni mawazo potofu. Haya ni mawazo ya kishetani. Hawa ni wauaji. Naomba Kanisa na madhehebu mengine ya dini na Watanzania wote wenye mapenzi mema waisaidie Serikali kulaani unyama huo, kulaani vitendo hivi vya kinyama na kusaidia wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kujibu makosa ya mauaji. Wanaofanya vitendo hivi vya kinyama, tunaishi nao, tunawafahamu, tunakula nao, tunacheka nao, tunasali nao na wakati mwingine kushirikiana nao. Kwa niaba ya Serikali, naomba tuwafichue waovu hawa. Kwa viongozi wote wa madhehebu mbalimbali ya dini na ninyi mliopo hapa na hasa, Maaskofu na Mapadre tusaidieni kukemea na hatimaye kutokomeza uovu huo. Kuendelea kwa maovu haya ni mmomonyoko mkubwa wa maadili na utu katika jamii na hasa Kanisa. Suala hili la mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ni changamoto ambayo sote inabidi kupigana nayo kwa kutumia silaha zote kama vile sala, maombi na sheria. Amani na Utulivu Tanzania Wahashamu Maaskofu, madhehebu yote ya dini yanaiombea nchi yetu amani na utulivu. Aidha, huwaombea viongozi wake wawe na afya njema na kubwa zaidi upendo, busara na hekima katika kuwaongoza wananchi. Tunawashukuru sana. Uko ukweli kwamba, nchi nyingi duniani zenye mafanikio ya uchumi imara ni kwa sababu ya kujiwekea misingi bora ya amani na utulivu. Aidha, uchumi imara ni matokeo ya juhudi za wananchi walizowekeza katika uzalishaji kutokana na uhakika wa uongozi imara na sera nzuri za uwekezaji. Kwa maana hiyo, kama tunataka uchumi imara ni lazima tuilinde nchi yetu idumu katika hali ya amani na utulivu wakati wote. Hata Vitabu Vitakatifu vinasema: Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote (Waeb. 12:14) Maadili Mema Wahashamu Maaskofu, Serikali inakabiliwa na changamoto ya kujenga maadili mema miongoni mwa watumishi wake, kwani yamekuwa yakiporomoka siku hadi siku. Moja ya changamoto hizo ni suala la rushwa. Rushwa ni tatizo ambalo wananchi wanakumbana nalo katika nyanja mbalimbali hususan katika utoaji wa huduma za jamii na uchumi na pia katika utendaji kazi wa Serikali. Rushwa ina athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Athari zitokanazo na vitendo vya rushwa ni nyingi na ipo mifano mingi. Kwa mfano, rushwa huathiri utekelezaji wa majukumu ya Serikali; hukwamisha utoaji wa haki na husababisha kuongezeka kwa maovu katika jamii. Aidha, rushwa husababisha wananchi kukosa imani na Serikali yao; wananchi hukosa huduma muhimu za kijamii na kusababisha kutolewa kwa huduma duni. Hizi ni baadhi tu ya athari nyingi zinazotokana na rushwa. Kutokana na athari hizi, ni dhahiri kwamba tunao

wajibu mkubwa katika kupambana na rushwa kwa nguvu zote. Katika kupambana na rushwa inabidi kufanya yafuatayo: (i) Kufuata sheria na taratibu kwa kuepuka njia za mkato kupata huduma ili kuepuka mianya ya rushwa; (ii) Kusimamia na kutathmini mipango ya maendeleo na kufuatilia fedha za miradi zinazotolewa na Serikali ili kuthibiti ubadhirifu wa fedha hizo; (iii) (iv) Kuwaelimisha Wananchi kutotoa wala kupokea rushwa; Kutowaonea aibu viongozi au watumishi wa umma wanaoomba na kupokea rushwa; (v) Kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola, kama TAKUKURU mara wanapotakiwa kutoa ushahidi. Kama wananchi wote watashirikiana kutekeleza hayo yote, ni dhahiri upo uwezekano wa kushinda vita dhidi ya rushwa. Tunaendelea kuchukua hatua za dhati kupambana na kuzuia rushwa. Mtakuwa mashahidi kwamba Serikali haipo kimya tu. Mapambano ya rushwa sio jambo la kufanya mara moja na kulimaliza, bali ni mchakato ambao unahitaji ushirikiano wa hali ya juu. Lakini jitihada zetu zinaonekana. ndio maana tumeshuhudia siku za hivi karibuni nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa yakisifu jitihada zetu katika mapambano haya. Ninyi Viongozi wa Dini mnayo nafasi kubwa ya kusaidia mapambano haya. Wahashamu Maaskofu, tunatambua kuwa kazi ya kupambana na rushwa sio ya Serikali peke yake. Aidha, baadhi ya wananchi wanaotoa na kupokea rushwa ni waumini wenu. Kushiriki katika rushwa ni matokeo ya ukosefu wa maadili mema. Hivyo, ninyi kama viongozi wa dini, mnayo nafasi nzuri ya kuijenga jamii katika maadili yanayokubalika ikiwemo kukataaa kushiriki katika kutoa na kupokea rushwa. Katika Methali 5:13 na 19, Mtume Paulo ameandika maneno ya Yesu akiwaambia Wanafunzi wake kwamba: Ninyi ni nuru ya Ulimwengu Nuru yenu na iangaze mbele za watu wapate kuyaona matendo mema, wamtukuze Baba yenu aliye Mbinguni. Tuungane na Mtume Paulo kwa tafsiri ya kuwatambua kuwa ninyi mmetumwa kueneza maadili ya kujenga watu kiroho.wito wangu kwenu nawaomba muisaidie Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa.mnalo kundi kubwa la waumini wanaowategemea. Tutumie fursa ya kuwa na kundi hili la waumini kuwapelekea habari njema za kiroho ili wawe na utamaduni wa kuwa na matendo mema kwa kutumia imani zao. Tuwakumbushe kuwa na matumaini ya maisha yenye maadili mema ya kiroho. Tuwajengee imani njema inayoambatana na matendo mema. Tukishirikiana Serikali na viongozi wa dini katika hili la maadili mema, tutajenga Taifa lenye watu waadilifu na hivyo kupunguza kero nyingi zinazoikabili jamii ya Watanzania.

Yuko mkulima mmoja ambaye alikuwa analima kwa jembe la kukokotwa na ng ombe wawili. Ng ombe mmoja mkubwa, lakini mzee na mwingine mdogo, lakini mwenye nguvu. Kila wakati jembe likikwama, mkulima yule anampiga yule ng ombe mzee anamwacha yule mdogo ambaye ndiye alikuwa anasababisha jembe kukwama kwa kujaribu kujinasua kwenye konga za jembe kila mara. Mpita njia akawa ameona kilichokuwa kinatendeka. Akamuuliza yule mkulima; Vipi bwana, mbona unamchapa huyo ng ombe mzee tu wakati anayesababisha jembe kukwama ni huyo mdogo? Mkulima yule akajibu: Aah! Nimempiga huyu mzee kwa sababu ndiye anayemfundisha huyu mdogo tabia mbaya!! Wahashamu Maaskofu, tumepewa dhamana kama viongozi kuwafundisha waumini wetu tabia nzuri zenye maadili mema. Tutumie nafasi hiyo vizuri. Ni kweli hatutapigwa mijeledi kama mkulima yule alivyokuwa anampiga ng ombe mzee, lakini tunaweza tukalaumiwa na wenzetu kwamba tulipewa jukumu la kuwaongoza, lakini hatujawaongoza vizuri. Vilevile, tusisahau kuwa tabia mbaya za vijana wetu kwa njia moja au nyingine zinatuathiri kama wazazi, au wanajamii. Tutumie nafasi ya uongozi wetu kuwafundisha vizuri waumini wetu na Wananchi wetu kwa ujumla kuhusu Maadili Mema. Wahashamu Maaskofu, hatuwezi kutenganisha dini na maendeleo ya watu. Hivyo, hatuwezi kutenganisha dini na umaskini. Lakini kwa kiasi fulani umaskini unaletwa na watu kutofanya kazi kwa bidii na maarifa, kutojituma na kutokuwa wabunifu. Tunahitaji kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupata maisha bora. Hakuna njia fupi na rahisi ya maisha bora. Natoa wito kwa viongozi wote nchini kuwaelimisha waumini na wananchi wao juu ya kufanya kazi kwa bidii. Mtusaidie kuwahimiza wajibidishe katika kazi zao kwa kutengeneza maisha yao yawe bora zaidi na hatimaye kuondokana na umaskini. Mwisho Wahashamu Maaskofu, kwa kumalizia, napenda nichukue fursa hii tena kulipongeza Kanisa Katoliki kwa ujumla kwa kuwa na ushirikiano mzuri na Serikali. Ushirikiano huu ni wa kihistoria. Naupongeza uongozi wa Kanisa kwa uamuzi wa kuwekeza katika maeneo ya huduma za jamii zikiwemo shule, vyuo, zahanati, n.k. Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa Katoliki, dini na madhehebu mengine katika kuwahudumia Watanzania. Lengo ni kutimiza kauli mbiu yetu ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania. Wahashamu Maaskofu, tumeshiriki kwa sala na ibada tangu tuanze maadhimisho haya. Tumeshuhudia mafanikio ambayo Kanisa limepata kwa nusu karne tangu Baraza hili lianzishwe. Tunamuomba Mungu azidi kulibariki Kanisa hili na viongozi wake wawe na afya njema, nguvu, hekima na busara ili waendelee kuwaongoza kondoo wake kwenye malisho mema.

Baba Askofu na Rais wa Baraza, Wahashamu Maaskofu, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Nawashukuru sana kwa kunishirikisha katika sherehe hii. Nawatakia nyote baraka tele za Mwenyezi Mungu. Mungu atubariki sote, Mungu alibariki Kanisa na waumini wake na Mungu Aibariki Tanzania!!